Habari

Wanahabari washajiishwa kuelewa ugatuzi kwa undani

September 5th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na LAWRENCE ONGARO

WAANDISHI wameshauriwa kuelewa maana ya ugatuzi ili wawe na ufahamu wanaporipoti maswala yake.

Mwanahabari mwenye uzoefu wa muda mrefu, Bw Kwamchetsi Makokha akiongoza awamu ya maswala ya ugatuzi kwenye kongamano la waandishi wa mashinani, Kenya Correspondents Association (KCA), amewashajiisha waandishi wa habari akiwataka wazamie na kuelewa ugatuzi kwa undani ili kuwa na ufahamu wanapoangazia maswala ya mashinani.

“Kabla ya kuripoti jambo lolote kuhusu ugatuzi, ni lazimu tuelewe maana yake ni nini. Ugatuzi ni kurudisha maswala ya uongozi mashinani; hasa katika mambo yanayomuathiri mwananchi moja kwa moja,” amesema Bw Makokha.

Amewahimiza waandishi kutumia vyombo vyao vya kazi kwa njia ifaayo wanapoelezea maswala ya ugatuzi.

Amewahimiza waandishi kuwa mstari wa mbele kufanya utafiti kamili kuelewa jinsi ugatuzi unavyostahili kuripotiwa kikamilifu.

Aidha, wamehimizwa kujizatiti na kuangazia maswala ya maendeleo ambayo wananchi walioko mashinani wanahusishwa.

Wanahabari waliohudhuria kongamano hilo ambalo lilianza Jumatano walitoa maoni yao; mengi kuhusu masaibu wanayopitia wanapotafuta habari za kaunti wanakotoka.

Maswala mengi yaliyoangaziwa ni jinsi wengi wao hupata shida wanapoingia kwenye ofisi za magavana.

Ujeuri

Wamesema baadhi ya maafisa walioajiriwa kwenye ofisi hizo ni wajeuri ambapo kupata habari yoyote huwa ni shida kubwa.

Waandishi wa mashinani wamehimizwa kushirikiana kuwa kitu kimoja wanapoendesha majukumu yao.

Katika mjadala huo wa ugatuzi waandishi walihimizwa kufanya utafiti kwa matukio yanayoendelea katika maeneo yao ili kuja na habari zilizo na maana na ukweli.

Wakati huo pia waandishi walihimizwa kuzingatia usalama wao wanapoendesha majukumu yao.

Ilibainika ya kwamba waandishi wengi wanafanya kazi yao bila kuelewa ya kwamba wako na maadui wengi wanaowawinda.

Wameshauriwa kuwa makini wasiingie kwa mtego wa kuandika habari za uongo na za kupotosha.

Wamenufaika kwa kupewa mwongozo kuhakikisha wanachunguza kwa undani habari zote wanazoandika na kuuliza maswala yafaayo kuambatana na maswala wanayoangazia.

DW Akademie ambayo imekuwa mshiriki kwenye kongamano hilo imetoa hakikisho kuwa iko tayari kufanya kazi kwa ushirikiano na KCA.

Jutta Vom Hofe wa DW Akademie, amesema shirika hilo liko tayari kushirikiana na vyombo vya habari ili kuelewa kwa undani masaibu wanayopitia waandishi wa habari.

Jutta Vom Hofe wa DW Akademie akihutubu. Picha/ Lawrence Ongaro

“Tayari tumezuru maeneo kadha ya hapa nchini kama Nairobi, Nakuru na Kisumu,” akasema Bi Hofe.

Amesema tayari wamefungua tovuti kwenye mtandao wa (RoggKenya) ambayo lengo lake kuu ni kusambaza habari muhimu ambazo zinahitajika kwa dharura.

Nalo shirika linaloangazia maswala ya kilimo (FAO) limefafanua mengi kuhusu jinsi linavyoshughulika kuinua kilimo katika kauti tisa hapa nchini.

Mwakilishi wa shirika hilo kwenye kongamano Bw Richard Bett amesema shirika hilo linashughulika na kusimamia ardhi na misitu ili kuhifadhi.

Baadhi ya Kaunti zinazoangaziwa na shirika hilo ni Turkana, Taita Taveta, Baringo, Nandi na Vihiga.

Ametajaka masaibu yanayokumba mkulima wa mashinani amabyo ni ukosefu wa vifaa muhimu vya kilimo.

“Baadhi ya maswala hayo yamekuwa kikwazo kikubwa kwa wakulima hao kujiendeleza zaidi katika upanzi ili nao wapate mavuno ya kuridhisha,” amesema Bw Bett.