Wanajeshi saba Gambia jela miaka tisa kwa kujaribu kupindua serikali
Na MASHIRIKA
BANJUL, Gambia
MAHAKAMA ya kijeshi imehukumu wanajeshi saba kifungu cha miaka tisa gerezani baada na kupatikana na hatia ya kupanga njama ya kuipindua serikali.
Mwanajeshi mwingine wa nane alihukumiwa kifungo cha miaka mitatu gerezani kwa kujaribu kumpindua Rais Adama Barrow.
Mahakama hiyo iliyoko katika eneo la Yundum, takriban kilomita 25 kutoka jijini Banjul, iliachilia huru wanajeshi wengine wanne baada ya kuwapata bila hatia.
Mkuu wa mahakama hiyo Kanali Salifu Bojang alisema wanajeshi hao walipanga njama ya kuwashambulia mawaziri na wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Gambia.
Mahakama pia ilisema wanajeshi hao walikuwa wakiwasiliana kupitia kikundi cha WhatsApp kuhusu mpango wao wa kutaka kushambulia kambi ya wanajeshi wa Muungano wa Mataifa ya Magharibi mwa Afrika (ECOMOG) wanaodumisha amani nchini Gambia.
Serikali ya Gambia tayari imeunda Tume ya Haki, Ukweli na Maridhiano kwa lengo la kuwapa haki waathiriwa walionyanyaswa na utawala wa miaka 22 ya Yahya Jammeh ambaye sasa anaishi mafichoni baada ya kubwagwa katika uchaguzi na Barrow.