Habari

Wanakandarasi ndio sumu ya kuchelewesha miradi ya kaunti- ripoti

Na JACKLINE MACHARIA October 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KUCHELEWESHWA kwa miradi, ukosefu wa uwezo na baadhi ya wanakandarasi kuitelekeza miradi ni miongoni mwa sababu kuu zinazofanya miradi ya kaunti ya thamani ya Sh9.1 bilioni kutokamilika, kulingana na ripoti mpya ya Mthibiti wa Bajeti (CoB) kwa mwaka wa kifedha 2024/2025.

Ripoti hiyo inaonyesha kuwa miradi 158 katika kaunti 18 imekwama, licha ya serikali za kaunti kutumia tayari Sh3.8 bilioni, huku zikihitaji Sh5.3 bilioni zaidi ili kukamilisha miradi hiyo.

Tatizo linalojitokeza zaidi ni wanakandarasi. Takwimu zinaonyesha kuwa karibu nusu ya miradi iliyokwama imesababishwa na changamoto zinazohusiana na wanakandarasi, ikiwemo kutelekeza miradi, kuchelewesha kazi au ukosefu wa uwezo wa kifedha na kiufundi.

Takwimu zinaonyesha kuwa takribani miradi 30 ilitelekezwa kabisa. Baadhi yake iliachwa mara tu baada ya kuanza, mingine katikati, na kuacha jamii zikiwa na shule, zahanati na masoko ambayo hayajakamilika.

Katika miradi mingine 15, wanakandarasi walikataa kuendelea hadi masharti mapya au fedha za ziada zitolewe. Miradi saba ilikwama kwa sababu kampuni zilizopata zabuni hazikuwa na uwezo wa kifedha au kitaalamu wa kuikamilisha.

Miradi mingine saba ilicheleweshwa kupita kiasi, huku minane ikimaliza muda wa kandarasi bila kazi yoyote kuanza. Katika miradi mingine saba, kandarasi zilifutwa kabisa kutokana na migogoro kati ya kaunti na wanakandarasi au utendakazi duni.

Kwa jumla, zaidi ya miradi 80, zaidi ya nusu ya yote ambayo imekwama, inahusiana moja kwa moja na matatizo ya wanakandarasi.

Hata hivyo, tatizo hili halihusiani tu na uzembe wa wanakandarasi bali pia linaonyesha mianya mikubwa katika mifumo ya kaunti, ikiwemo upungufu katika taratibu za ununuzi, usimamizi hafifu, na siasa katika utoaji zabuni.

Ripoti ya Mkaguzi Mkuu  wa Hesabu za Serikali imesisitiza mara kadhaa kwamba kaunti zimekuwa zikitoa kandarasi  kwa kampuni zisizo na sifa, mara nyingi zinazohusishwa na watu wenye ushawishi, ambazo hushindwa kukamilisha kazi au kutoa huduma duni.

Mnamo Agosti, ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali  ilionyesha kuwa kaunti 33 zilikuwa na miradi 248 iliyokwama ya thamani ya zaidi ya Sh20 bilioni katika mwaka wa kifedha 2023/2024.

Kaunti ya Machakos iliongoza kwa idadi ya miradi 54 ya thamani ya Sh314 milioni, ikifuatiwa na Nyandarua ikiwa na miradi 43 ya thamani ya Sh403.9 milioni iliyokwama. Kaunti ya Kakamega iliongoza kwa thamani, miradi yake iliyokwama ikifikia Sh8.1 bilioni, ikifuatiwa na Nairobi ambapo miradi ya kima cha Sh2.4 bilioni  imekwama huku Trans Nzoia ikiwa na miradi miwili yajumla ya Sh2.1 bilioni ambayo imekwama

Ripoti pia ilionya kuwa baadhi ya takwimu hizo huenda si kamili, kwani baadhi ya kaunti hazikuwasilisha data kamili.

Mkaguzi Mkuu Nancy Gathungu alionya kuwa miradi mingi iliyokwama sasa inakabiliwa na adhabu kutokana na ucheleweshaji wa malipo. Kaunti zinadaiwa na wanakandarasi mamilioni kwa kazi zilizokamilika, huku zingine zikikabiliwa na kesi baada ya kuvunjika kwa mikataba.