Wananchi 164,000 kuajiriwa kutekeleza shughuli ya sensa
Na SHAREEN MBEYU, GAITANO PESSA na KNA
SERIKALI itaajiri zaidi ya watu 164,000 kuendesha shughuli ya kuwahesabu watu kote nchini (sensa) kati ya Agosti 24 na 25 mwaka 2019.
Matangazo ya kuwaalika watu waliohitimu kwa kazi mbalimbali wakati wa shughuli hizo yatawekwa katika vyombo vya habari mwishoni mwa wiki ijayo.
Serikali itawaajiri watu 135,000, kama vibarua, watakaoendesha kazi ya kuhesabu watu, wasimamizi 27,000 wa data na jumla ya watu 2,700 kama wasimamizi wa Teknolojia ya Habari.
Utaratibu wa kuajiri watu hao utaanza Juni 28 hadi Julai 18.
Akiongea katika mkutano wa kwanza wa Kamati ya Sensa katika kaunti ya Nyeri, afisa wa wafanyakazi katika Shirika la Takwimu Nchini (KNBS) Pauline Waweru alisema kando na wafanyakazi hao wa kuendesha sensa, serikali pia itawaajiri wazee wa vijiji na washirikishi watakaosaidia kufanikisha zoezi hilo.
“Maafisa wengi wa usalama pia watatumiwa kuhakikisha kuwa shughuli hiyo itaendeshwa katika mazingira salama,” afisa huyo aliongeza.
Bi Waweru alisema tofauti na sensa ya mwaka wa 2009 ambayo iliendeshwa kwa njia ya kawaida kutumia karatasi, teknolojia ya habari na mawasiliano itatumiwa katika ukusanyaji na uchanganuzi wa data kuhakikisha kuwa takwimu sahihi zinapatikana.
Afisa huyo alisema kuwa tayari Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT) na kile cha Moi, Eldoret vimepewa kibarua cha kutengeneza tableti zitakazotumiwa wakati wa shughuli hiyo.
“Matumizi ya teknolojia ya kisasa yanalenga kuzima njama ya watu fulani kuingilia shughuli hiyo kwa lengo la kutoa hesabu za kupotosha kuendeleza malengo yao kibinafsi. Muhimu zaidi ni kwamba tunalenga kuisaidia serikali kupata data sahihi itakayotumia kupanga shughuli za maendeleo na utoaji huduma kwa wananchi,” akasema Bi Waweru.
Akiongea katika mkutano huo, Kamishna wa Kaunti ya Nyeri David Kipkemei alisema afisi yake imejitolea kufanikisha shughuli hiyo kwa kutoa ulinzi kwa vifaa vyote vitakavyotumika katika sensa hiyo.
Na katika kaunti ya Busia, Kamishna wa Kaunti Jacob Narengo aliwahakikishia watu watakaoendesha sensa hiyo kwamba watapewa usalama wa kutosha.
“Tunawahakikishia maafisa wote wa sensa kwamba tutawapa usalama sawa na vifaa vya kazi hiyo vimehifadhiwa mahala salama. Maafisa wa usalama watakuwa chonjo kukabiliana na visa vyovyote vya utovu wa usalama,” akasema.
Wadau
Bw Narengo alisema hayo Ijumaa katika mkutano wa wadau kutoka ngazi za kaunti, serikali ya kitaifa na mashirika ya umma katika makao makuu ya kaunti hiyo.
Afisa huyo wa utawala alitoa wito kwa vyombo vya habari na asasi zingine husika kuendeleza hamasisho kuhusu zoezi hilo ili lifikie malengo yatakayokuwa yenye manufaa kwa wakazi na taifa kwa jumla.
Wakati huo huo, kamati ya sensa katika kaunti ya Mombasa ilizinduliwa Ijumaa.
Kulingana na Kamishna wa Kaunti hiyo Evans Achoki, kamati hiyo yenye wanachama 15 itasimamia shughuli hiyo katika ngazi za kaunti ndogo na wadi.
Bw Achoki alikuwa ameandamana na Meneja wa Takwimu katika shirika la KNBS Abdulkadir Awes na Afisa wa Sensa katika kaunti ya Mombasa Beuter Nyamongo.
Alisema shughuli ya kuwaajiri maafisa wa kuendesha sensa hiyo itaanza kati ya tarehe 11 na 24 mwezi huu katika kaunti ya Mombasa.