Habari

Wandani wa Ruto wadai kufungiwa nje ya Jubilee Asili

November 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 3

ONYANGO K’ONYANGO na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto na wandani wake sasa wamelazimika kusitisha mipango yao ya kutumia jumba la Jubilee Asili kama kituo cha kushirikisha kampeni zake za 2022, wakidai mmiliki wa jengo hilo aliwafurusha.

Wandani wa Dkt Ruto wanasema kuwa mmiliki wa jengo hilo, lililoko mtaani Kilimani, Nairobi, amewaagiza waondoke kwa sababu anatishwa na maafisa fulani wakuu serikalini.

“Tunazungumza na mmiliki wa jengo hilo kwa sababu serikali imemwambia atufurushe. Ametuagiza tuondoke lakini tumekuwa tukijadiliana naye kwa miezi miwili sasa. Hii ndio maana tuliamua kusimamisha mikutano yetu kwa muda huku tukitafuta muafaka kuhusu suala hilo,” akaeleza mbunge mwanachama wa kundi la ‘Tangatanga’ ambaye alioamba tulibane jina lake.

Naye Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, aliambia Taifa Leo kwamba walilazimika kusitisha shughuli katika jumba hilo “kwa sababu ya vitisho vya kila mara kutoka kwa serikali.”

“Tulifunga Jubilee Asili Centre, kwa sababu mmiliki wake alidai amekuwa akipokea vitisho na shinikizo kutoka kwa maafisa fulani wakuu serikali atamatishe mkataba nasi. Anadai kuwa uwepo wetu hapo unasababisha kelele nyingi na kwamba jumba hilo halifai kutumiwa kwa shughuli za kisiasa kwani linaweza kuharibiwa,” akasema Bw Barasa.

Hata hivyo Mbunge huyo alisema hawezi kumtambua mmiliki wa jengo hilo kwa sababu kundi la Tangatanga lilikodisha jumba hilo kupitia ajenti wakajua mmiliki wake baadaye.

Kundi la Tangatanga lilianza kutumia jumba la Jubilee Asili Centre mnamo mwezi wa Juni mwaka huu kupanga mkakati yake ya kumpigia debe ndoto ya Dkt Ruto ya kuwania urais 2022.

Mnamo Juni 19, Naibu Rais aliongoza mkutano wa wabunge 20 wandani wake katika jumba hilo, katika kile kilichoonekana kama uzinduzi rasmi wa jumba hilo.

Hatua hiyo iliibua tetesi kwamba huenda walitaka kuunda chama kipya na kugura Jubilee kwani Dkt Ruto pia alizindua kaulimbiu mpya ya “Sote Pamoja” badala ya “Tuko Pamoja” ya Jubilee.

Dkt Ruto aliandaa mkutano huo siku moja baada ya Spika wa Bunge la Kitaifa Justin Muturi kuidhinisha kuondolewa kwa jumla ya wabunge 16 wa mrengo wa Tangatanga kutoka nyadhifa za uongozi bungeni na kwenye kamati zake.

Aliyekuwa kiongozi wa wengi katika Seneti Kipchumba Murkomen alidai kuwa kambi yao ililazimika kufungua afisi mpya baada ya wao kuzimwa kutumia makao makuu ya Jubilee, mtaani Pangani.

“Tulikutana na Naibu Rais katika Jubilee Asili Centre. Ni kituo cha wanachama wote, bali sio kituo sambamba. Ni kituo cha wanachama wa Jubilee ambao bado wanazingatia maadili asilia ya Jubilee,” akasema Seneta huyo wa Elgeyo Marakwet.

Lakini mnamo Oktoba 1, 2020, Dkt Ruto alifika katika makao makuu ya Jubilee, akiandama na wabunge 38 wandani wake, bila notisi, na kufanya mkutano uliodumu kwa saa mbili katika kile kilichoonekana kama jaribio lake la kudhibiti chama hicho.

Hatua hiyo iliwakera wandani wa Rais Uhuru Kenyatta walioitaja kama “mapinduzi” kwani ilifanyika rais akiwa ziarani nchini Ufaransa, madai ambayo wanachama wa ‘Tangatanga’ walikana.

“Naibu Rais kama Naibu Kiongozi wa Jubilee ana haki ya kufika katika makao makuu ya chama chetu na kuendesha shughuli zozote zenye manufaa kwa wanachama,” akasema Seneta Mithika Linturi.

Duru ziliambia Taifa Leo kwamba ni wakati huo ambapo kundi la ‘Tangatanga’ lilipata habari kwamba mmiliki wa Jubilee Asili Centre anapanga kuwafurusha.

Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju aliitisha kikao na wanahabari na kutangaza kupingwa marufuku kwa Dkt Ruto na wandani wake kutumia makao makuu ya Jubilee “kuendeshea mikakati yake ya urais 2022.”

“Vile vile, Baraza la Kitaifa la Usimamizi (NMC) limependekeza kwa Baraza Kuu (NEC) kwamba Naibu Rais akome kuhudumu kama naibu kiongozi waa chama baada ya kuzindua afisi za Jubilee Asili, hadi suala hilo litakapojadiliwa katika NEC,” akaongeza Bw Tuju.

Lakini juzi, Mbunge wa Soy Caleb Kositany, alielezea matumaini kwamba wanaendelea na shughuli za kuhakikisha kuwa Jubilee Asili Centre inaanza kufanya kazi “hivi karibuni.

“Kituo cha Jubilee Asili kitaanza kushuhudia shughuli nyingi hivi karibuni kwa sababu tunaendelea kuweka mipango yetu tayari. Hizo habari kwamba tunafurushwa hazina mwelekeo,” akaeleza.