Wangusi kuendelea kuwa kinara wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini
Na RICHARD MUNGUTI
MAHAKAMA Kuu imeamuru Ijumaa kwamba mkurugenzi mkuu wa Mamlaka ya Mawasiliano nchini (CA) Francis Wangusi aendelee kuhudumu katika wadhifa huo hadi mwingine ateuliwe kwa mujibu wa sheria.
Na wakati huo huo, Jaji Byram Ongaya amefutilia mbali uteuzi wa Bi Mercy Wanjau kama kinara wa CA akisema “hakukuwa na baraza halali ya kumteua mkurugenzi mkuu kutwaa mahala pa Bw Wangusi.”
Jaji Ongaya amemtaka Rais Uhuru Kenyatta kutumia mamlaka yake kuwateua wanachama wa bodi ya wakurugenzi wa CA watakaomteua Mkurugenzi Mkuu mpya kutwaa mahala pa Bw Wangusi ambaye muda wake wa kustaafu umewadia.
Jaji huyo ametaka Rais Kenyatta amwongezee muda Bw Wangusi wa kuhudumu hadi bodi ya wakurugenzi itakapoteua kinara mpya wa mamlaka hii ya mawasiliano.
Jaji Ongaya amefutilia mbali uteuzi wa Bi Wanjau akisema “ uteuzi wake haukuwa na mashiko kisheria.”
Mahakama ilimtaka Bw Wangusi asipeane hatamu za afisi hiyo kwa Bi Wanjau hadi wakati ule Rais Kenyatta atakapoteua bodi mpya ya wakurugenzi itakayoteua mkurugenzi mkuu mpya badala ya yule anayeondoka.
“Rais anatakiwa kutumia mamlaka yake chini ya sheria za taasisi za serikali kuteua bodi mpya itakayotekeleza jukumu la kumteua Mkurugenzi mpya,” alisema Jaji Ongaya.
Jaji huyo alimwongezea muda wa kuhudumu Bw Wangusi.
Bodi ya CA ilikuwa imemteua Bi Wanjau kutwaa mahala pa Bw Wangusi.
Uamuzi huo wa mahakama umetokana na kesi aliyowasilisha mwanaharakati Okiya Omtatah na shirikisho la waajiri?
Katika kesi hiyo mahakama ilifahamishwa muda wa Bw Wangusi wa kuhudumu kama kinara wa CA ulikuwa haujatamatika.
Mahakama iliamuru washtakiwa walipe asilimia 50 ya gharama ya kesi hiyo.
Awali mahakama ya kuamua mizozo ya wafanyakazi ilikuwa imeamuru shughuli ya kumteua kinara mwingine wa CA isitishwe huku uamuzi wa korti kuhusu uteuzi wa Bi Wanjau ukisubiriwa.
Wangusi aliteuliwa mnamo Agosti 2012.