Habari

Wapakiaji maji ya chupa waitaka serikali iondoe ushuru

November 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na CHARLES WASONGA

CHAMA cha Watayarishaji wa Maji ya Chupa (WBAK) kimeitaka serikali kuondoa ushuru kwa maji ya chupa, kwani utachangia kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

Kinasema kupanda kwa bei ya maji ya chupa kutawaathiri Wakenya wengi wanaoyategemea hasa wawapo nyumbani, safarini na katika shughuli nyinginezo muhimu.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari iliyotumwa Ijumaa, mwenyekiti wa WBAK Henry Kabogo amesema chama hicho kitalazimika kupitisha gharama ya ushuru huo kwa watumiaji bidhaa hiyo ikiwa serikali itaendelea na mipango yake ya kutoza ushuru huo wa Sh5.40 kwa kila lita ya maji kuanzia Novemba 13, 2019.

“Serikali ikiaza kutoza ushuru huu, bila shaka bei ya lita 20 ya mtungi wa maji safi yaliyopakiwa itapanda hadi kati ya Sh450 na Sh550 kutoka kati ya Sh250 na Sh350,” amesema Bw Kabogo.

WBAK ndicho chama kinachowakilisha waendeshaji biashara ya maji safi ya chupa na mitungi maalum ya plastiki na hata wauzaji wa maji kote nchini.

Bw Kabogo amesema wanachama wao wametimiza masharti ya Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa (KEBS) na Mamlaka ya Utozaji Ushuru Nchini (KRA) kuhusiana na masuala ya ushuru na leseni za kuhudumu.

“Lakini inavunja moyo kwamba serikali haitekelezi kikamilifu changamoto zinazokabili biashara yetu,” akasema.

Bw Kabogo ameeleza kuwa chama hicho kinapinga utozaji wa ushuru wa uuzaji unaofanywa kwa bidhaa kama sigara na pombe kwa sababu maji sio bidhaa ya starehe bali ni ya kimsingi.

Amesema kuwa wanachama wake wako tayari kulipa aina zozote za ushuru kulingana na sheria zilizowekwa na KRA.

Mswada wa Fedha 2019 uliotiwa saini na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Alhamisi unapendekeza kwamba maji ya chupa na vinywaji vitamu kama soda sasa vitaanza kutozwa ushuru wa uuzaji (exercise duty) kuanzia Novemba 13, 2019.