Wapiganaji wa al-Shabaab wawaua wenzao wawili katika kituo cha polisi Wajir
Na MANASE OTSIALO
WAPIGANAJI wa al-Shabaab wameshambulia kituo cha polisi cha Dadajabula, Wajir Kusini na kuua wanachama wake wawili waliokuwa wakizuiliwa ambapo katika makabiliano, maafisa watatu wamejeruhiwa.
Mtawala mmoja ameambia Taifa Leo kwamba wapiganaji hao walivamia kituo hicho usiku mkuu kuamkia Jumatano wakiwa wamejihami vilivyo, wakiwa na gruneti zenye uwezo mkubwa wa maangamizi.
Afisa wa serikali ambaye hakutaka jina lake litajwe kwa sababu hana idhini ya kuzungumzia suala kama hili kwa wanahabari amesema walitekeleza uvamizi huo kituoni wanachama wake wawili walipokamatwa na wakawa wanazuiliwa.
Chanzo kutoka polisi kinasema kituo hicho kilikuwa kinawazuilia washukiwa wa ugaidi na kwamba wavamizi walitaka kuwaokoa wanachama wao.
“Wavamizi walitaka kuwaokoa wenzao wa al-Shabaab waliokuwa wanazuiliwa kituoni,” afisa huyo amesema.
Maafisa wa polisi walijibu uvamizi huo ambapo makabiliano na milio ya risasi ilisikika kwa takribani dakika 20.
Mtumiaji mmoja wa mtandao wa kijamii wa Twitter alitumia jukwaa hilo kuelezea kilichokuwa kinaendelea.
“Kunasikika milio ya risasi… Hata vilipuzi vyenye uwezo mkubwa vinarushwa huku maafisa wa usalama na hata wanajeshi wakikabiliana na wavamizi,” akaandika Ali Awdoll kwenye Twitter.
Imebainika kwamba makabiliano yalipositishwa, tayari wavamizi walikuwa wamewaua wanachama wao wawili na kujeruhi maafisa wawili wa polisi na mwingine wa kitengo cha ziada.
Chanzo kinasema yumkini wavamizi waliua washukiwa hao kituoni kuficha baadhi ya taarifa na habari kuhusu al-Shabaab.
“Tunashuku wametaka kuficha habari za siri na muhimu kwa kundi la al-Shabaab,” chanzo hicho kimesema.
Raia ambaye hajatambuliwa bado pia amepata majeraha wakati wa makabiliano hayo.