Habari

Washauri wa Ruto motoni kwa dai walidharau korti na ‘kuendelea na kazi’

Na JOSEPH WANGUI January 28th, 2026 Kusoma ni dakika: 1

WASHAURI wakuu wawili wa Rais William Ruto, mtaalamu wa uchumi David Ndii na Mshauri wa Haki za Wanawake Harriet Chiggai, wanakabiliwa na kesi wakidaiwa kudharau mahakama.

Hii ni kutokana na uamuzi wa Mahakama Kuu wiki iliyopita uliobatilisha uteuzi wao pamoja na washauri wengine 19 wa rais, kwamba kuanzishwa kwa ofisi nyingi za ushauri kulikuwa kinyume cha katiba.

Katika kesi iliyowasilishwa kwa dharura jana, Shirika la Katiba Institute, mlalamishi katika kesi ya awali, inaomba mahakama kupata kwamba Ndii na Chiggai walidharau korti. Shirika hili linadai kuwa machapisho yao kwenye X yalikataa wazi amri ya korti.

Kesi hiyo inasema kuwa Bw Ndii alichapisha maneno yaliyoonyesha kejeli kwa uamuzi, ikiwa ni pamoja na: “Hatuhitaji ofisi za serikali kushauri rais. Tunaweza kufanya hivyo wakati wa staftahi kila asubuhi na “Sheria inapogongana na siasa, siasa huibuka mshindi. Kila wakati.” Katiba Institute inasisitiza kuwa maneno hayo yalionyesha kuwa maamuzi ya mahakama yako chini ya mamlaka ya kisiasa.

Chiggai analaumiwa kwa kupakia picha siku moja baada ya uamuzi, ikionyesha akihudhuria hafla ya umma.

Mlalamishi anasema hili lilionyesha kwamba uamuzi wa mahakama unaweza kupuuzwa, jambo linaloweza kudhoofisha imani ya umma katika mfumo wa sheria.

Katika kesi yake shirika linasema kuwa washauri wote wawili walijua kuhusu maagizo ya mahakama, ambayo yalitolewa hadharani, kuripotiwa sana, na kusikilizwa mbele ya mawakili wa Serikali na kuonya kuwa kupuuza mamlaka ya kisheria kunaweza kudhoofisha imani ya umma na kuweka mfano hatari.