Washirika wa Gachagua wapinga mashtaka ya ugaidi
WATU thelathini na saba, wakiwemo washirika wawili wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, watajua Alhamisi iwapo watashtakiwa kwa makosa yanayohusiana na ugaidi.
Hakimu wa mahakama ya Kahawa, Gideon Kiage, aliamuru kwamba Peter Kinyanjui maarufu kama “Kawanjiru”, Serah Thiga na watu wengine 35 wazuiliwe hadi Julai 10, siku ambayo ataamua ikiwa watashtakiwa chini ya Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Washukiwa, kupitia kwa mawakili wao wakiongozwa na aliyekuwa makamu wa rais Kalonzo Musyoka, walipinga mashtaka hayo wakisema ni kinyume cha katiba.
Watu hao 37 walikamatwa kufuatia maandamano ya Juni 25 yaliyofanyika kuadhimisha mwaka mmoja tangu maandamano ya kizazi cha Gen Z, dhidi ya Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.
“Kutokana na uzito wa hoja zilizowasilishwa, mahakama inahifadhi uamuzi wa ombi hilo hadi Julai 10. Kwa sasa, washukiwa wataendelea kuzuiliwa katika vituo vya polisi wanakozuiliwa,” alisema Bw Kiage.
Watu hao walikamatwa kutokana na maandamano ya Juni 25, na upande wa mashtaka ulisema wao ndio waliohusika na uharibifu wa majengo kadhaa ya umma ikiwemo mahakama ya Kikuyu na ofisi ya naibu kamishna wa eneo hilo.
Upande wa mashtaka ulitaka washtakiwe chini ya kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi.
Hata hivyo, walikataa kujibu mashtaka hayo huku Bw Musyoka akidai kuwa serikali inatumia sheria ya ugaidi kama silaha ya kuwanyanyasa vijana waliokuwa wakieleza haki zao za kidemokrasia.
“Mashtaka haya yamelenga kuwatisha raia wanaothubutu kukosoa serikali,” alisema Bw Musyoka.
Upande wa mashtaka ulidai kwamba waliharibu na kuchoma ofisi mbalimbali za umma, zikiwemo ofisi za elimu na za mhasibu wa eneo, ofisi ya chifu wa Kikuyu, ofisi za msajili wa watu, msajili wa ardhi na kituo cha polisi cha Dagoretti kosa linalodaiwa kufanywa tarehe 25 Juni.
Mashtaka hayo yalidai kuwa watu hao walihusika katika matendo yaliyoratibiwa na ya uharibifu, yenye lengo la kuleta hofu na kudhoofisha mamlaka ya serikali.