Habari

Washukiwa wanne wa wizi wa magari kukaa jela siku 7

Na RICHARD MUNGUTI April 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

POLISI wamekubaliwa kuzuilia washukiwa wanne wa genge la wezi wa magari jijini Nairobi na viunga vyake.

Hakimu mwandamizi Mahakama ya Milimani Robinson Ondieki aliamuru Jumatano kwamba Mutua John Julius, George Nyakundi, Simon Mugo Chege na Raphael Oloo Kira wazuiliwe katika kituo cha polisi cha Parklands kwa siku saba.

Hakimu Ondieki alisema polisi wamewasilisha ushahidi wenye mashiko ya kisheria kumwezesha kuamuru washukiwa hao wasukumwe rumande ili kuhojiwa.

Akiwasilisha ombi hilo, afisa anayechunguza kashfa hiyo ya magari Konstebo Sammy Shamalla alisema magari mengi yametoweka kabisa baada ya kuripotiwa kuibwa.

Aliomba Bw Ondieki awape polisi muda wa kufanya uchunguzi wa kina.

Afisa huyo wa polisi alieleza mahakama kwamba washukiwa wakuu wamehusika katika utengenezaji nambari feki za usajili wa magari, kufuta nambari halisi za usajili za magari husika na kuendeleza kiwanda cha kukatakata magari kwa vipande vipande na kisha kuuza vipuri jijini Nairobi na kaunti zingine.

Akitoa uamuzi Hakimu Ondieki alisema: “Washukiwa hawa wanne hawajapinga ombi la polisi kuwazuilia kwa siku saba uchunguzi ukamilishwe. Ninaruhusu polisi kuwaweka korokoroni kwa siku saba.”

Agizo la kuwazuilia wanne hao lilitokana na ufichuzi wa Shamalla kwamba mnamo Machi 22, 2025 Bw
Benedict Musiko, mmiliki wa kampuni ya kukodisha magari ijulikanayo kama Given Tours & Safaris, alipiga ripoti kuwa gari lake limeibwa.

Gari aina ya Toyota Axio. PICHA | MAKTABA

Katika ripoti hiyo Bw Musiko alisema mnamo Mach1 19, 2025 alimkodishia William Mugecha Ngugi gari lenye nambari ya usajili KDR 722K aina Toyota Axio kwa siku tatu.

“Baada ya siku hizo tatu Ngugi hakurudisha gari. Musiko alipiga ripoti gari lake limeibwa,” Shamalla alimweleza Hakimu Ondieki.

Machi 21, 2025 Bw Musiko alijaribu kusaka gari hilo akitumia kifaa cha kiteknolojia cha kufuatilia – tracker kwa Kimombo – lakini hakufanikiwa. Kifaa hicho kilikuwa kimezimwa.

Bw Musiko kisha akamtafuta ajenti aliyemfamisha kwa Ngugi lakini hakumpata kwa simu maana ilikuwa imezimwa.

Akaongeza Shamalla: “Uchunguzi wa muda uliishia kwa gari kupatikana na washukiwa kadhaa kuandikisha taarifa kwa polisi.”

Mahakama ilielezwa kuwa mnamo Aprili 3, 2025 gari la Bw Musika  – KDR 722K – lilipatikana limeachwa eneo la Joska, Ruai likiwa limewekwa nambari feki ya usajili KDM 697Z.

Mutua, Nyakundi, Chege na Kira walikamatwa. Uchunguzi ulibaini Mutua na Nyakundi wamebobea katika uhalifu wa kughushi vitambulisho na kuvitumia kuiba magari.

“Mutua na Nyakundi waliiba kitambulisho cha William Mugecha na leseni ya kuendesha gari. Kisha wakaenda kukodisha gari kutoka kwa Given Tours & Safaris. Hatimaye wakaliwekea nambari feki ya usajili,” korti iliambiwa.

Isitoshe, nambari halisi ya usajili ya gari hilo la Given Tours & Safari’s ilifutwa.

Polisi wanatarajiwa kufika katika afisi za Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama (NTSA) kubaini nambari halisi za usajili ambazo polisi walizipata na washukiwa hao wanne.

Kesi hiyo itatajwa Aprili 14, 2025 kwa maagizo zaidi.