Habari

Wastaafu wateseka KRA na Wizara zikizozana

Na LYNET IGADWAH November 8th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAELFU ya wafanyakazi wanaostaafu kazi za serikali, wakiwemo walimu, wamezuiliwa kupata marupurupu yao ya uzeeni kutokana na mvutano unaoendelea kati ya Wizara ya Fedha na Mamlaka ya Ukusanyaji wa Mapato Kenya (KRA) kuhusu utozaji ushuru malipo ya pensheni.

Mvutano huo unatokana na sheria mpya iliyorekebishwa mwezi Desemba mwaka jana, ambayo iliondoa kodi kwenye malipo ya pensheni, kinyume na utaratibu wa awali ambapo pesa za wastaafu zilikuwa zikitozwa ushuru.

Wizara ya Fedha inasisitiza kuwa wastaafu wote ambao malipo yao hayakuwa yamekamilika kufikia wakati msamaha huo wa ushuru ulipoanza wanapaswa kunufaika nao.
Hata hivyo, KRA inadai kuwa msamaha huo unapaswa kuanza kutumika tu kwa malipo yaliyotolewa baada ya Desemba 27, 2024, tarehe ambayo marekebisho hayo yalitekelezwa rasmi.

Tangu wakati huo, maafisa wa Idara ya Pensheni katika Wizara ya Fedha na wenzao wa KRA wamekuwa wakifanya mikutano na mawasiliano kadhaa, lakini hawajafikia mwafaka wowote. Hali hiyo imewaacha maelfu ya wastaafu katika mateso na wasiwasi kwa miezi kadhaa — licha ya Rais William Ruto kuagiza katika hotuba ya Siku ya Wafanyakazi mwaka huu kwamba pensheni zote zisitotozwe ushuru.

Waziri wa Fedha, Bw John Mbadi, alithibitisha kuwepo kwa mzozo huo, akisema kumefanyika mikutano kadhaa ya maafisa wakuu wa sera kutoka wizara yake na uongozi wa KRA.

“Lengo la mikutano hii ni kufikia makubaliano ya pamoja kuhusu jinsi msamaha wa ushuru wa malipo ya pensheni utavyotumika kwa visa ambavyo vilikuwa bado havijashughulikiwa wakati sheria mpya ilipoanza kutumika,” alisema Bw Mbadi.

Aliongeza kuwa suala la ushuru kwenye malipo ya uzeeni limekuwa likijadiliwa kwa kina kati ya Wizara ya Fedha, KRA na taasisi nyingine za serikali tangu kupitishwa kwa Sheria ya Marekebisho ya Ushuru ya 2024 na baadaye Sheria ya Fedha ya 2025.

Sheria hiyo, iliyotiwa saini Desemba 11, 2025, na kuanza kutumika Desemba 27, 2024, ilitoa msamaha wa ushuru kwa malipo ya pensheni yanayotolewa kupitia miradi iliyosajiliwa kisheria.
Marekebisho hayo yalilenga kuongeza pesa mikononi mwa wastaafu na kuwalinda dhidi ya gharama kubwa za maisha wanapostaafu.

“Wizara imekuwa ikijadiliana na KRA kuhakikisha utekelezaji wa msamaha huu unalingana na nia ya marekebisho ya 2024, tukizingatia misingi ya usawa na nidhamu ya kifedha,” aliongeza Bw Mbadi.

Alifafanua kuwa kutokana na tafsiri tofauti za sheria hiyo, Idara ya Pensheni iliamua kusitisha kwa muda mchakato hadi itakapopata ufafanuzi rasmi.

Huku mvutano huo ukiendelea, mamia ya faili za wastaafu zimekwama katika jengo la Bima House, makao makuu ya Idara ya Pensheni.
Wastaafu waliozungumza na Taifa Leo walisema wamekuwa wakirudi mara kwa mara katika afisi hizo bila majibu kamili, wakipewa tu matumaini kwamba “suala  hilo linashughulikiwa.”

David Thaguambi, mwalimu aliyestaafu Julai 1, 2024, alisema amekwama katikati ya mvutano huo.

“Sijapokea hata senti moja tangu nistaafu. Wote wanadai hawajui kama watanilipa bila ushuru au watakataa msamaha huo. Wakati huo huo, bili zangu zinaendelea kuongezeka,” alisema kwa huzuni.

Alisema wenzake waliostaafu kabla ya Desemba 2024 tayari wamepokea malipo yao bila kukatwa ushuru, jambo linalozidisha mkanganyiko.

Kwa wengine, hali ni ya kusikitisha zaidi. Christopher Kileta, mwalimu aliyefariki mwaka 2023, mjane wake bado hajalipwa marupurupu yake na anaendelea  kutaabika kifedha, akisubiri bila mwanga wa matumaini.

Kepha Mshambala, Katibu Mkuu wa Chama cha Ustawi wa Wastaafu na Wanaokaribia Kustaafu (REAR) kinachowakilisha zaidi ya wanachama 6,000 waalimu wastaafu, aliikosoa serikali kwa kushindwa kushughulikia hali hiyo.

“Kukaa kimya huku pesa za wastaafu zikizuiliwa ni kuwatupa wazee hawa katika umaskini. Wamehudumia taifa kwa miaka mingi, sasa wanapaswa kuishi kwa heshima,” alisema Bw Mshambala.

Alipendekeza kwamba Idara ya Pensheni iache kuchelewesha malipo na ianze kuyalipa kwa sasa, hata ikiwa ni kwa kukatwa kodi, kisha baadaye serikali ifanye marejesho iwapo itabainika kuwa wanastahili msamaha.

“Wastaafu hawa wana watoto wanaohitaji karo, wana bili za hospitali, na mahitaji ya msingi. Kuwanyima haki yao ni sawa na kuwazika wakiwa hai,” alisema.