Watahiniwa 52 wa KCSE waambukizwa corona shuleni
Na WAANDISHI WETU
WANAFUNZI 52 wa Kidato cha Nne katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Kolanya Salvation Army, Kaunti ya Busia, wameambukizwa virusi vya corona.
Katika shule hiyo hiyo, walimu wanne na wafanyakazi wawili pia walipatikana kuugua ugonjwa huo wa Covid-19.
Afisa Mkuu wa Afya katika Kaunti, Dkt Isaac Omeri alisema, walioambukizwa walitengwa ili watibiwe katika sehemu moja shuleni na wanaendelea kupata nafuu.
Alisema maambukizi hayo yaligunduliwa wakati maafisa wa afya walipochukua vipimo vya waliokuwa shuleni.
“Maafisa wetu wanaendelea kukagua shule ili watambue jinsi maambukizi yalisambaa ndipo hatua mwafaka zichukuliwe,” akaeleza.
Katika Kaunti ya Kilifi, bunge limefungwa kwa siku 14 baada ya afisa mmoja kupatikana na virusi vya corona.
Akizungumza na wanahabari, spika wa bunge hilo Jimmy Kahindi, alisema kuwa, waliamua kusitisha vikao vya bunge hilo ili kutoa muda zaidi kwa maafisa na wafanyikazi wengine kupimwa kama waliambukizwa pia.
Hata hivyo, Kahindi alisema kuwa wafanyikazi hao pamoja na wawakilishi wa wadi katika bunge hilo watalazimika kutekeleza majukumu yao wakiwa nyumbani.
Rais Uhuru Kenyatta leo anatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kwa vile idadi ya maambukizi na vifo ilipanda kwa kasi katika mwezi wa Oktoba. Hata hivyo, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) Mwachonda Chibanzi alisema tayari msambao wa corona uko kila mahali na marufuku ya kutoingia wala kutotoka baadhi ya kaunti moja hakutadhibiti hali hiyo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utafiti wa Kimatibabu, Afrika (Amref) Githinji Gitahi alisema marufuku ya usafiri italeta madhara zaidi kwa uchumi wa nchi. “Kile ambacho serikali inapasa kufanya ni kuimarisha masharti ya kupunguza mtagusano wa wananchi na hivyo kudhibiti kiwango cha maambukizi,” akasema kwenye mahojiano ya simu.
Kwingineko Mombasa, Kamishna wa Kaunti, Bw Gilbert Kitiyo alisema maafisa wa polisi wataendelea kushika doria ili kuhakikisha wakazi wote wanafuata kanuni za kukabiliana na virusi vya corona.
Ripoti za Benson Amadala, Alex Amani, Winnie Atieno na Charles Wasonga