Watatu wakamatwa kwa kujaribu kuingia kambi ya mazoezi ya Jeshi la Uingereza mjini Nanyuki
Na NICHOLAS KOMU
MAAFISA wa polisi wanawazuilia washukiwa watatu waliojaribu kuingia katika kambi ya mazoezi ya Jeshi la Uingereza eneo la Nanyuki mnamo Jumapili.
Washukiwa hao wanazuiliwa wakishukiwa kuwa na mafungamano na mitandao ya ugaidi.
Mshirikishi wa eneo pana la Rift Valley George Natembeya amethibitisha Jumatatu asubuhi kwamba watatu hao walikamatwa Jumapili jioni na kwamba wanahojiwa na wapelelezi.
Lengo lao kutaka kuingia kwa lazima katika kambi hiyo ya Kitengo cha Mazoezi ya Jeshi la Uingereza nchini Kenya (BATUK) halijabainika hasa ingawa inashukiwa walikuwa wanafanya upelelezi.
“Walijaribu kuingia kwa lazima lakini hawakufua dafu na walikamatwa mara moja. Walikuwa na kamera tu, lakini tunawahoji kubainisha ukweli,” Bw Natembeya amesema kwa simu.
Kulingana na ripoti, watatu hao walijaribu kuingia kambini wakashindwa lakini kamera za siri zikawa zimenasa tukio hilo.
Ni hapo ndipo maafisa katika kambi hiyo walisambaza picha hizo za video na maafisa wa humu nchini wakasaidia kwa kuwakamata washukiwa.
Walikamatwa saa kumi na moja jioni karibu na kituo cha polisi cha Nanyuki ambacho kiko mita chache kutoka ilipo kambi ya BATUK.
Polisi hawajatoa rasmi utambulisho wa washukiwa lakini maafisa wa ngazi ya juu – kulingana na ripoti zilizopo – wanakutana mjini Nanyuki.