Habari

Watengenezaji vileo nchini wapinga mswada mpya wa kuthibiti unywaji pombe

Na KABUI MWANGI November 7th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

WATENGENEZAJI wa vileo nchini wamekosoa mswada mpya unaolenga kudhibiti zaidi uzalishaji na uuzaji wa pombe, wakionya kuwa mapendekezo hayo yanaweza kufuta maelfu ya ajira, kupunguza mapato ya serikali na kukuza biashara ya pombe haramu.
Chama cha Watengenezaji wa Vileo nchini (ABAK) kinasema kupandisha umri wa chini wa kunywa pombe kutoka miaka 18 hadi 21 kunaweza kusababisha sekta za rejareja na ukarimu kupoteza mapato ya Sh3.3 bilioni kila mwaka.
Aidha, serikali inaweza kukosa Sh1.8 bilioni za ushuru huku ajira 8,960 na maduka 1,792 yaliyo na leseni kuwa hatarini kufungwa, kwa mujibu wa makadirio ya chama hicho.
Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Vileo na Udhibiti wa Dawa za Kulevya wa 2026 uliwasilishwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Kitaifa Alhamisi, Novemba 5, na sasa unasubiri kujadiliwa na wabunge.
Miongoni mwa mapendekezo yake ni kupandisha umri wa chini wa kununua na kunywa pombe hadi miaka 21, kuzuia uuzaji wa vileo katika maduka makubwa na maeneo mengine, kupiga marufuku mauzo kupitia mtandao na usafirishaji wa pombe hadi nyumbani, pamoja na kutoza ushuru wa Sh2 kwa kila lita ya pombe inayotengenezwa nchini au kuagizwa kutoka nje.
Mwenyekiti wa ABAK, Kui Kinyanjui, alisema mapendekezo hayo yanaweza kudhoofisha kampuni halali zinazotengeneza na kusambaza pombe huku yakifungua mianya kwa wauzaji wa bidhaa haramu.
“Wakati ambapo sekta yetu tayari inakabiliwa na changamoto kubwa kutoka kwa wauzaji wa pombe haramu, mswada huu unaweza kudhoofisha biashara halali na kutoa nafasi zaidi kwa pombe haramu kustawi,” alisema.
Aliongeza kuwa hatua hizo zitaathiri maelfu ya wafanyakazi, uwekezaji uliopangwa na mapato ya serikali, huku zikiwaweka watumiaji katika hatari kubwa zaidi.
Chama hicho pia kinapinga pendekezo la kutoza Sh2 kwa kila lita ya pombe, kikisema hatua hiyo itawaongezea watengenezaji halali gharama ya takriban Sh1.3 bilioni kila mwaka.
 Kwa mujibu wa ABAK, ushuru huo unaweza kuongeza bei ya pombe inayouzwa kihalali na kufanya bidhaa hizo kuwa ghali ikilinganishwa na pombe haramu inayouzwa kwa bei ya chini bila kulipa ushuru.
Kinyanjui alitaka Bunge lisitishe mswada huo ili kutoa nafasi ya mashauriano na wadau kabla ya kuidhinisha mabadiliko hayo.
“Tunahimiza kuwepo kwa mashauriano ya wazi yanayohusisha serikali za kaunti, wasimamizi wa sekta, wataalamu wa afya ya umma na wadau wote katika biashara ya pombe,” alisema.
Alisema lengo la pamoja linapaswa kuwa kulinda watumiaji, kuhifadhi ajira na kukabiliana kikamilifu na pombe haramu.
Hatua hii inajiri wakati ambapo biashara ya pombe haramu imeendelea kuwa changamoto kwa kampuni halali na serikali, ambayo hupoteza ushuru kutokana na bidhaa zinazouzwa nje ya mfumo rasmi.
 Utafiti wa Euromonitor wa mwaka 2025 ulioagizwa na ABAK ulikadiria kuwa pombe haramu ilichangia asilimia 60 ya pombe yote iliyotumiwa nchini kwa wingi mwaka 2024. Kiasi cha pombe hiyo kiliongezeka kwa asilimia 27 kati ya 2022 na 2024.
Utafiti huo pia ulikadiria kuwa serikali ilipoteza takriban Sh120 bilioni za mapato ambayo ingeweza kukusanya mwaka 2024 kutokana na biashara ya pombe haramu, ikiwemo ya magendo, bidhaa bandia na ukwepaji wa ushuru.
Mamlaka ya Kupambana na Bidhaa Bandia pia imehusishwa katika mijadala kuhusu matokeo hayo, huku watengenezaji halali wakilalamikia bidhaa haramu kuchukua sehemu kubwa ya soko.
ABAK inaonya kuwa kuzuia uuzaji wa pombe katika maduka makubwa, mikahawa na mitandao kunaweza kufanya bidhaa halali kuwa ngumu kupatikana, huku wauzaji haramu wakiendelea kufanya biashara nje ya mfumo wa leseni na ushuru.
Mnamo Julai 2025, serikali ilizindua sera ya kitaifa ya kuzuia, kudhibiti na kusimamia matumizi ya pombe na dawa za kulevya. Sera hiyo ilipendekeza umri wa chini wa kushughulikia, kununua, kunywa na kuuza pombe uwe miaka 21.
Serikali imetetea pendekezo hilo ikisema linalenga kulinda afya ya umma na kupunguza uwezekano wa vijana kuanza kutumia pombe na dawa za kulevya wakiwa na umri mdogo.
Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Dawa za Kulevya (NACADA) imeeleza wasiwasi kuhusu unywaji wa pombe miongoni mwa wanafunzi wa vyuo vikuu.
Utafiti wa NACADA wa mwaka 2025 kuhusu wanafunzi wa vyuo vikuu ulionyesha kuwa asilimia 87.3 ya waliohojiwa walikuwa wakitumia pombe, na kuifanya kuwa bidhaa inayotumiwa zaidi miongoni mwa wanafunzi hao.