Habari

Kalonzo ataka uchunguzi wa kina kuhusu ghasia za Linda Mwananchi Homa Bay

Na GEORGE ODIWUOR November 7th, 2026 Kusoma ni dakika: 2

KIONGOZI wa Wiper Patriotic Front (WPF) Kalonzo Musyoka amepinga idadi rasmi ya watu waliouawa wakati wa ghasia zilizozuka katika mkutano wa Linda Mwananchi mjini Homa Bay Agosti 16, akitaka uchunguzi maalum wa umma kubaini idadi kamili ya waliofariki na waliohusika na mauaji hayo.

Bw Musyoka anadai kuwa idadi ya walioangamia ni kubwa zaidi kuliko ile iliyotangazwa na polisi. Ingawa ripoti rasmi zilitaja watu wanne kufariki, kiongozi huyo wa upinzani anasema uchunguzi wao umeonyesha kuwa idadi hiyo imeongezeka na kuzidi kumi.

“Tumebaini kuwa idadi imeongezeka. Tunatoa wito wa kuanzishwa kwa uchunguzi maalum ili kubaini kilichotokea na waliohusika na mauaji haya, kwa sababu nchi haiwezi kuendelea hivi,” alisema.

Ghasia hizo zilitokea wakati Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna, Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino na viongozi wengine wa vuguvugu la Linda Mwananchi walipokuwa wakielekea mjini Homa Bay baada ya kufanya mikutano ya kisiasa Nyandiwa na Sindo.

Vijana waliokuwa wamejihami kwa silaha, yakiwemo mapanga, waliripotiwa kuziba barabara kwa mawe na kuwatishia waliotaka kupita.

Miongoni mwa waliofariki alikuwa afisa wa polisi kutoka Muhoroni aliyekuwa akiwasafirisha wenzake kutoa msaada kwa maafisa wenzao.

Mfanyabiashara mwenye asili ya Uganda pia alifariki baada ya kugongwa na magari yaliyokuwa yakipita kwa kasi alipokuwa akivuka barabara.

Akizungumza akiwa Homa Bay Ijumaa, baada ya msafara wake kushambuliwa Migori siku iliyotangulia, Bw Musyoka alidai tukio la Homa Bay ni mauaji ya halaiki yanayopaswa kuchunguzwa badala ya kufichwa.

Alisema kaunti hiyo imekuwa ikiitwa kwa dharau “Afghanistan” na “Yemen” kutokana na visa vya mauaji, akitaka hali hiyo ikomeshwe.
“Hatuwezi kufanya Homa Bay iendelee kuwa uwanja wa mauaji ya watu wasio na hatia. Kaunti hii ni sehemu ya Kenya, na hatuwezi kuendelea kuruhusu hali hii,” alisema.

Alikuwa ameandamana na viongozi wengine wa upinzani, akiwemo Justin Muturi, Eugene Wamalwa, Mbunge wa Nyali Mohamed Ali na Raphael Tuju.

Viongozi hao walisema hawatakubali fidia ya pesa pekee kwa waathiriwa wa ghasia za kisiasa. Bw Musyoka alisema jopo la wataalamu kuhusu fidia kwa waathiriwa wa maandamano na mikutano ya umma, linaloongozwa na Profesa Makau Mutua, linakamilisha ripoti yake.

Baada ya ripoti hiyo, Tume ya Haki ya Kurejesha Hali ya Kawaida waliyoanzisha, inayoongozwa na Bw Muturi, itachukua hatua zaidi za kudai haki.

“Hauwezi kuwapa watu pesa tu. Hauwezi kulipia maisha ya binadamu. Lazima kuwe na haki pamoja na fidia. Bado tutawafuata kudai haki. Haki lazima itendeke kwa mashujaa wote walioangamia,” alisema.

Aidha, Kalonzo na kikosi chake wanapanga kutangaza Juni 25 kuwa Siku ya Kitaifa ya Uwajibikaji, itakayoadhimishwa kila mwaka kwa maandamano ya kumbukumbu. Walisema watafanya siku hiyo kuwa rasmi iwapo wataingia mamlakani mwaka ujao.

Kuhusu vurugu za Migori, Bw Musyoka alidai kuwa shambulizi dhidi ya msafara wake lilikuwa limepangwa, akiwalaumu viongozi wa eneo hilo kwa kulipa vijana waliorushia magari yao mawe huku polisi wakirusha vitoa machozi.

Bw Muturi alisisitiza kuwa viongozi hao wana haki ya kikatiba kutembelea maeneo yote nchini na hawatatishwa na wahuni wanaodaiwa kuajiriwa kuvuruga mikutano yao.

Bw Wamalwa alisema kurushwa kwa mawe na matumizi ya vitoa machozi kwa wakati mmoja kulionyesha kuwa huenda polisi walikuwa wakishirikiana na washambuliaji.

“Unapoona serikali na wahuni wakishirikiana, basi hatuna serikali tena. Tulichonacho ni serikali ya wahuni,” alisema.

Mbunge Mohamed Ali alitaja tukio la Migori kuwa jaribio la kuwaua viongozi wa upinzani, akisema mawe makubwa yaliyolenga magari yao yangeweza kusababisha majeraha mabaya.

Bw Tuju alisema timu hiyo haitarudi nyuma kutokana na vitisho, akiwalaumu wanasiasa wa eneo hilo kwa kutumia vijana wasio na ajira kuchochea ghasia za kisiasa.