Watoto 12 wazaliwa Kaunti ya Kirinyaga sikukuu ya Krismasi
KULIKUWA na sherehe Kirinyaga baada ya watoto 12 kuzaliwa Siku ya Krismasi.
Baadhi ya akinamama waliojifungua walieleza furaha yao kwa kuwapata watoto siku hiyo inayoenziwa ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
“Ni baraka na furaha yangu kujifungua mtoto wakati ulimwengu unaadhimisha kuzaliwa kwa Yesu Kristo,” mmoja wa akinamama hao akasema.
Wale ambao walihojiwa waliwashukuru madaktari na wauguzi kwa kuwashughulikia vizuri kuhakikisha wanajifungua salama.
“Wahudumu wa afya walifanya vizuri na tumefurahi,” akasema Mama mwengine.
Katika Hospitali ya Kirinyaga, akina mama walisema walijifungua katika wadi ya kisasa ya hospitali hiyo waliyosema ina vifaa vyote vya kujifungua salama.
Watoto hao walizaliwa Hospitali za Kaunti ya Kerugoya, Kianyaga, ACK Mt Kenya, Mwea Mission, Kiangai, Baricho na South Ngariama.
Watoto sita waliozaliwa walikuwa wavulana huku wengine wakiwa wasichana.
Kwa mujibu wa Mshirikishi wa Masuala ya Matibabu wa Kaunti Hesbon Gakuo, watoto wote waliozaliwa wapo hali nzuri kiafya.