Habari

Watoto waliookolewa msituni Shakahola waeleza ndoto za kutisha

Na BRIAN OCHARO May 24th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWANASAIKOLOJIA ameelezea kwa kina madhila ya kiakili waliyopitia watoto waliokolewa kutoka kwa mauaji ya Shakahola miaka mitatu tangu waokolewe kutoka kwenye dhehebu hatari lililoongozwa na mhubiri tata, Paul Nthenge Mackenzie.

Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkuu Nelly Chepchirchir katika Mahakama ya Watoto ya Tononoka, Dkt Florence Mueni, alieleza hali ya kusikitisha ya msongo wa mawazo waliobeba watoto hao tangu waokolewe.

Dkt Mueni alisema watoto hao walionesha dalili kali za kiwewe zilizosababishwa na njaa ya muda mrefu, kutengwa, kufundishwa imani potovu, na kupoteza jamaa zao wa karibu.

“Wanaota ndoto za kutisha mara kwa mara na mawazo ya kushuhudia watu wakifa. Walieleza kwa huzuni wanapokumbuka masaibu hayo, ikiwemo kufungwa kwenye mti,” alisema Dkt Mueni akimrejelea baadhi ya wanusurua.

Dkt Mueni alikuwa miongoni mwa timu ya wataalamu wa afya ya akili waliojitolea kuwasaidia watoto 13 waliokolewa kutoka msitu wa Shakahola baada ya kupitia mateso makubwa chini ya uongozi wa Mackenzie.

Alisema watoto walieleza kuwa walizuiwa kuomboleza vifo vya wapendwa wao waliokufa kwa njaa. Wengi walipatwa na huzuni nzito na msongo wa mawazo wa muda mrefu. Mvulana mmoja alishuhudia kaka yake akifariki mbele yake—tukio lililoacha makovu ya ndani yasiyofutika.

“Baadhi ya watoto walionesha hofu, hasira, aibu, na kupoteza hamu ya vitu walivyovipenda hapo awali,” alisema mtaalamu huyo akiongozwa na Kiongozi wa mashtaka Jami Yamina, Betty Rubia, miongoni mwa wengine.

Aliongeza kuwa njaa na kutengwa kwa muda mrefu kulisababisha mwitikio wa ‘kuporomoka’—hali ambapo mwili unazima unapohisi hatari kubwa. Watoto wengi mwanzoni walikuwa waoga kupindukia, hasa jina la Mackenzie lilipotajwa.

“Hofu yao ilikuwa kubwa sana, jambo lililodhihirisha athari za kina alizowaachia. Hata hivyo, baada ya miezi kadhaa ya tiba na msaada wa kisaikolojia, wengi wao walianza kupona na kurejea shule na hata hali ya kawaida,” alisema.

Mkuu wa Upelelezi Kigen Sawe na Sajenti Livingstone Lihanda kutoka Kitengo cha Uchunguzi wa Kisayansi cha DCI waliwasilisha picha na video za kutisha kutoka eneo la tukio, ikiwemo vibanda vya kufungiwa, mali zilizoachwa, na makazi ya muda.

Afisa Mkuu wa Watoto, Sebastian Muli Muteti, alieleza jinsi walivyowaokoa watoto waliokuwa dhaifu, wameshushwa lishe, na wenye majeraha. Timu yake ilipata watoto wanne wakiwa ndani ya msitu wakiwa na mavazi machafu na alama za kupigwa.

“Watoto hao walieleza mateso waliyopata kutoka kwa walinzi wa Mackenzie waliokuwa wakiwapiga na kuwaweka kifungoni,” alisema.

Mahakama pia ilisikia ushahidi kutoka kwa wakuu wa shule wawili waliothibitisha kutoweka kwa wanafunzi waliokuwa wamepelekwa Shakahola.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Mtopanga, Bw Omari Omari, alisema msichana mmoja alitoweka mwaka wa 2018. Bw Mathew Maroko Samoita kutoka shule ya kibinafsi Kisauni, alisema mwanafunzi wa Darasa la Tatu aliondolewa na wazazi wake ambao sasa wanakabiliwa na mashtaka.

Watoto hao baadaye walitoa ushahidi dhidi ya walezi wao, wakidai waliteswa na kunyimwa haki ya elimu huku wakilazimishwa kufuata mafundisho ya dhehebu hilo.

Paul Mackenzie na wenzake wanakabiliwa na mashtaka kadhaa ikiwemo ukatili kwa watoto, mateso ya kisaikolojia, na kuwanyima watoto haki zao za masongo ya msingi.