Upasuaji wabaini wauaji walitwaa baadhi ya viungo vya Jackline Ruguru
UCHUNGUZI wa mwili wa Jackline Ruguru, mwanafunzi wa Chuo cha Embu umefichua ukweli wa kutisha kuhusu kilichosababisha kifo chake.
Kwa mujibu wa daktari wa uchunguzi wa maiti, Dkt Peter William, Jackline Ruguru aliuawa kwa kunyongwa kabla ya mwili wake uliokuwa na majeraha ya kutisha kutupwa kwenye shamba la kahawa eneo la Ngotho.
Sehemu kadhaa za mwili wake ikiwemo mkono wa kulia na titi, zilikatwa na hadi sasa hazijapatikana.
Pia, mfupa unaounganisha shingo uliondolewa na haujapatikana, ishara kwamba aliuawa kwa unyama wa hali ya juu.
Dkt William alisema kuwa kichwa chake “kilikuwa kimebakia mifupa,” na sampuli zimechukuliwa kubaini ikiwa kuoza kulikuwa kwa kawaida au kuliharakishwa kwa kutumia kemikali.
Familia ya marehemu imesema bado imesongwa na mshtuko kutokana na yaliyompata binti yao.
“Sisi tumeumia sana na tunataka ukweli ujulikane,” alisema mjomba wake, Bw Simon Njeru.
Jackline, mwanafunzi wa Chuo cha Embu mwenye umri wa miaka 22, aliondoka nyumbani kwao Ngiriambu mnamo Novemba 16, 2025 kuelekea mjini Kianyaga kununua losheni ya mwili — safari ambayo ilikuwa ya mwisho kuonekana akiwa hai.
Wiki moja baadaye, mwili wake uliokuwa ukioza ulipatikana ukiwa uchi katika shamba la kahawa Gichugu, baadhi ya viungo vikiwa vimeondolewa, na kuzua hofu kuwa huenda wauaji wake ni wanachama wa dhehebu hatari. Hata hivyo, haijabainika mara moja kwa nini aliuawa kwa ukatili huo.
Wazazi wake walisema kuwa binti yao aliwasili nyumbani Jumapili kutokea chuoni, lakini siku hiyo hiyo akaenda Kianyaga kununua losheni na akaahidi kurudi jioni. Alipokosa kurudi, familia ilimtafuta kila mahali bila mafanikio.
Baada ya siku saba, wanakijiji walikumbana na mwili wake na kutoa taarifa kwa kituo cha polisi cha Kianyaga.
Kamanda wa polisi wa Kirinyaga Mashariki, Bw Johnson Wachira, alisema uchunguzi unaendelea kubaini sababu ya mauaji hayo ya kikatili.
“Hatuw ezi kusema sababu ya mauaji kwa sasa, lakini uchunguzi utaeleza ukweli,” alisema Bw Wachira.
Familia sasa inalia kutaka haki, wakisema Jackline alikuwa msichana mpole ambaye maisha yake yalikatizwa kinyama.