Wazee waachiwa jukumu la kuokoa machifu waliotekwa na Al-Shabaab Mandera
JUKUMU la kuwaokoa machifu watano waliotekwa nyara na washukiwa wa kundi la kigaidi la Al-Shabaab, Mandera, Februari 3, sasa lipo mikononi mwa jamii eneo hilo.
Haya yamejiri baada ya Rais William Ruto, alipokuwa Mandera, kumwagiza Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli, kuongoza oparesheni ya uokoaji.
“Niko hapa na Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi Gilbert Masengeli na nimemwagiza ahakikishe tumewarejesha machifu hao,” Rais Ruto alieleza umati kwenye Uwanja wa Moi, Mandera mnamo Februari 4, 2025.
Alisema, “Mashariki au Magharibi ni sharti tusuluhishe suala hili kwa sababu tumezorotesha pakubwa uwezo wa Al-Shabaab kuwavamia watu wa Kaskazini mwa Kenya.”
Wiki tatu sasa zimepita na vikosi vya usalama havijashughulika mno kuwasaka machifu hao.
“Bado hatujawapata machifu wetu,” alisema Kamishna wa Kaunti ya Mandera, Bw Henry Ochako.
Machifu waliotekwa nyara wanajumuisha Mabw Adawa Abdi Mohmed, Mohamed Hassan Kulumia, Mohmednur Hache, Abdi Hassan Suraw na Ibrahim Gabow.
Bw Ochako alisema wazee wa jamii za eneo hilo wanashauriana na wanamgambo katika juhudi za kuwaachilia huru machifu.
“Jamii inajadili kuhusu kuachiliwa kwao na serikali haina wajibu katika harakati hizo kwa sababu hatujadiliani na magaidi,” alisema.
Kulingana na Bw Ochako, vikosi vya usalama vinashughulika kuimarisha usalama katika mpaka na Somalia.
Jamaa wa machifu waliotoweka wamechukulia kimya cha serikali kuhusu suala hilo kama kuwasaliti maafisa waliojitolea kazini.
Bw Masengeli hakupatikana wala kujibu simu tulizompigia.
Hata hivyo, msemaji wa polisi, Bw Micheal Muchiri, alisema mkuu wake anashirikiana na wizara za usalama wa ndani na masuala ya kigeni kuwarejesha machifu Mandera.
“Suala linalohusu machifu waliotoweka ni zaidi ya uwezo wa polisi lakini Naibu Inspekta Jenerali Masengeli anawasiliana na wizara za usalama wa ndani na masuala ya kigeni,” alisema Bw Muchiri kupitia mawasiliano ya simu.
Afisa mkuu wa mawasiliano katika wizara ya usalama wa ndani, Bw Julius Sigei, alisema suala hilo linaweza kujibiwa tu na Katibu wa Wizara, Dkt Raymond Omollo.
Jamaa wa mmoja wa machifu hao aliyezungumza na Taifa Leo akichelea kutajwa, alisema wazee eneo hilo tayari wametumwa mashinani Somalia.
“Tuna habari jamaa zetu wamezuiliwa Jilib karibu na Kismayo, Somalia kulingana na habari tulizopokea kufikia sasa,” alisema.
Mji wa Jilib ulianzishwa katika miaka ya 1980 na upo umbali wa kilomita 400 kutoka Mandera. Mji huo ulichipuka kufuatia ujenzi wa bwawa la kuzalisha nishati la Fanoole.
Bwawa hilo lilijengwa kusambazia stima Jilib, Marerey, Jamaame na miji mingine iliyopo nyanda za chini za Jilib.
Lilipangiwa kunyunyizia maji ardhi ikiwemo hekta 8, 000 za miwa na hekta 5, 000 za mpunga.
Ukuaji wa mji huo umekwama tangu bwawa hilo linalomilikiwa na serikali pamoja na mradi wa unyunyiziaji huku kundi la al-Shabaab linalohusishwa na Al-Qaeda likigeuza mji huo kuwa makao makuu.
Jumanne, polisi walisema walitibua njama ya Al-Shabaab kuteka nyara raia wa kigeni wanaohudumu kaunti ya Mandera.