Waziri atua Ruiru kukabili changamoto za wakazi kupata hatimiliki
Na LAWRENCE ONGARO
WAKAZI wa Ruiru wamepewa hakikisho kuwa matatizo yao ya umiliki wa vipande vya ardhi yatasuluhishwa hivi karibuni.
Waziri wa Ardhi Bi Farida Karoney alisema Jumatatu matatizo yanayohusu vipande vya ardhi katika eneo la Ruiru yamekuwa donda dungu na yanastahili kumalizwa mara moja.
“Nimepata malalamishi mengi ya umiliki ardhi kutoka Ruiru na kwa hivyo nimekuja leo kuyatatua,” alisema Bi Karoney.
Aliwashauri watu wote walio na kesi za ardhi mahakamani kuyaondoa ili kuyajadili nje ya mahakama.
“Tutashirikiana pamoja na Kaunti ya Kiambu ili kutatua maswala nyeti ya ardhi eneo hili,” alifafanua waziri huyo.
Aliwashauri wale wote wanaotaka kununua vipande vya ardhi mahali popote wafanye uchunguzi kwanza ili kujua ni nani na ni wapi unakonunua ardhi hiyo.
Alisema wizara hiyo inapanga kuweka data zote kwenye mtandao ili kuwazuia matapeli kuingiza ujanja katika stakabadhi.
Alieleza kuwa ifikapo mwaka wa 2020 kila jambo linalohusika na maswala ya ardhi litahifadhiwa kidijitali.
Alieleza kwamba wafanyakazi wote walio katika ofisi yake watavalia sare rasmi za kazini, beji na nambari ya kitambulisho cha kazi ili kuwatambua haraka mtu akitaka usaidizi.
“Ninawashauri kuwa wakati wowote unapotafuta usaidizi usitoe hongo kabisa,” alisema waziri.
Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ ara alisema kuna eneo kubwa la ekari 50 katika mji wa Ruiru linalotaka kupewa cheti maalum cha umiliki ili lifanyiwe shughuli za kimaendeleo.
Idadi kubwa
Alitaka shule ya msingi ya Mwiki eneo la Githurai itengewe ekari mbili za ujenzi ili kutosheleza idadi kubwa ya wanafunzi zaidi ya 3,000.
Alipendekeza ekari moja itengwe kwa ujenzi wa kituo cha polisi halafu ekari mbili zitengwe kwa kituo cha polisi cha Gatong’ora.
Alipendekaza pia ekari tano zitengwe kwa ajili ya kujenga viwanda vidogo vitakavyosaidia vijana kupata ajira.
Mbunge huyo alipendekaza ekari mbili litengwe kwa ujenzi wa shule ya upili ya wasichana.
“Mimi furaha yangu leo ni kuona ya kwamba Wizara ya Ardhi imekubali kuzuru mji wa Ruiru na kutatua shida zinazohusu umiliki wa vipande vya ardhi; shida ambazo zimekuwa hapa kwa zaidi ya miaka 40,” alisema Bw King’ara.
Waziri msaidizi wa Wizara ya Ardhi, Bw Gideon Mung’aro alisema maafisa wake watapiga kambi mjini Ruiru kwa muda wa mwezi mmoja na kila mwananchi mwenye shida ya ardhi amepewa nafasi kuwasilisha malalamishi yake huko.
“Yeyote aliye na shida ya ardhi afike kwenye ofisi ya ardhi Ruiru ili apate usaidizi. Hiyo itasaidia kumaliza utata ambao umeshuhudiwa kwa muda mrefu,” alisema Bw Mung’aro.
Diwani wa Kahawa Wendani, Bw Cyrus Omondi, alisema eneo lake la uwakilishi lina ekari nne ambazo zimenyakuliwa na alitaka wizara kuingilia kati.
“Mimi ningeomba ardhi hiyo iliyonyakuliwa irejeshwe kwa umma mara moja,” alisema Bw Omondi.
Alisema yeye kama kiongozi katika eneo hilo atafanya juhudi kuona ya kwamba ardhi ya umma inalindwa vilivyo.