Waziri Mkuu ni lazima – Raila
Na WANDERI KAMAU
KIONGOZI wa Chama cha ODM, Bw Raila Odinga amesisitiza njia pekee ya kusitisha taharuki na uhasama wa kikabila kila baada ya Uchaguzi Mkuu wa miaka mitano, ni kuwepo kwa mfumo wa utawala wa Bunge ambapo kutakuwa na Waziri Mkuu mwenye mamlaka makubwa ya uongozi.
Kauli yake imejiri huku Jopo la Maridhiano (BBI) alilounda pamoja na Rais Uhuru Kenyatta, likitarajiwa kutoa mapendekezo kuhusu mageuzi ya katiba wakati wowote kabla Oktoba 23.
Kulingana na waziri huyo mkuu wa zamani, ni mfumo huu ambao utafanikisha kuondoa ushindani mkali wa mamlaka ambao husababisha mgawanyiko kitaifa miongoni mwa jamii tofauti na hata kuleta umwagikaji damu.
Anaamini mfumo wa utawala wa Bunge utaleta uwianio, hata baada ya uchaguzi bila taharuki yoyote ya kisiasa.
Alikuwa akizungumza Jumanne kwenye uzinduzi wa kitabu ‘Presidential or Parliamentary Democracy in Kenya? Choices to be Made’ (Mfumo wa Demokrasia wa Urais ama Ubunge Nchini Kenya? Maamuzi Yanayopaswa Kufanywa) katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
“Mfumo wa Bunge utapanua uwakilishi wa wananchi serikalini ili kuhakikisha kila jamii inahisi kujumuishwa kwenye utaratibu wa utawala wa nchi. Mfumo wa urais haujatusaidia hata kidogo,” akasema Bw Odinga.
Duru zilisema kuna mgawanyiko katika BBI, ambapo kundi moja linataka kuwe na pendekezo la kuandaa kura ya maamuzi kwa marekebisho ya katiba lakini kundi jingine linataka marekebisho yoyote yatakayopendekezwa yaweze kufanywa na Wabunge.
Kulingana na wachanganuzi wa siasa, marekebisho ya katiba yanayoweza kufanywa bungeni ni yale tu ambayo yatapendekeza mfumo mzima wa utawala ubadilishwe.
Hii ni inamaanisha, iwapo kuna wasiotaka refarenda, ni kwa vile wanapendekeza mamlaka ya rais yaendelee kuwa makuu.
Hata hivyo, wakili Paul Mwangi, ambaye ni mmoja wa makatibu kwenye jopo hilo alikanusha madai ya mgawanyiko, akisema wako faraghani kukamilisha ripoti yao.
“Kwa sasa tunaendelea na matayarisho ya ripoti yetu kuhusu maoni yaliyotolewa na Wakenya kuhusu mageuzi ya kikatiba wanayohitaji. Siwezi kuelezea zaidi,” akasema kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Mfumo mzima
Kulingana na Prof Peter Kagwanja ambaye ni mchanganuzi wa masuala ya siasa, kura ya maamuzi inaweza kuandaliwa tu ikiwa mapendekezo yatakayotolewa yatahusu mageuzi ya mfumo mzima wa utawala.
“Hitaji la kura ya maamuzi litamaanisha jopo litatoa mapendekezo ya kubadilisha mfumo mzima wa katiba,” akasema.
Katika hafla ya Jumanne usiku, waandani wa Bw Odinga pia walisifia mfumo wa waziri mkuu mwenye mamlaka makubwa, wakisema utawezesha Kenya kustawisha mfumo wa ugatuzi.
Magavana Anyang’ Nyong’o (Kisumu), Kiraitu Murungi (Meru), mbunge wa zamani wa Imenti ya Kati Gitobu Imanyara kati ya wengine walisema Kenya inahitaji mfumo huo kwa sasa.
“Ni dhahiri kuwa tangu kupitishwa kwa katiba ya sasa mnamo 2010, mfumo wa urais haujatufaa hata kidogo, kwa kuwa umeongeza siasa za chuki na kikabila. Wakati umewadia kwa kukumbatia mfumo ambao unajenga dhana ya usawa kwa kila mmoja,” akasema Prof Nyong’o ambaye ni mwandishi wa kitabu hicho.