Waziri na mwigizaji wa zamani Ken Ambani awindwa na madiwani kwa dai la utendakazi duni
WAZIRI wa Michezo katika Kaunti ya Mombasa Kenneth Ambani roho mikononi baada ya wawakilishi wa wadi kutishia kuwasilisha hoja ya kumbandua madarakani kwa madai ya kuwanyima walemavu fedha za michezo.
Waziri huyo wa Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir anadaiwa kuwakosesha watu wenye mahitaji maalum fedha zilizotengwa kuwawezesha kushiriki katika mashindano ya michezo jijini Nairobi.
Diwani wa Wadi ya Shanzu, Allen Katana, aliyeapa kuwaislisha hoja hiyo alisema idara ya Bw Ambani ilikuwa miongoni mwa zile zilizofanya vibaya zaidi katika utendakazi wao.
Wawakilishi wa wadi walidai kuwa licha ya kutengewa fedha, walengwa, hasa watu wenye ulemavu, wamekuwa wakinyimwa ufadhili huo.
Walitaja tukio la hivi majuzi ambapo timu ya watu wenye mahitaji maalum ilinyimwa msaada wa kifedha ili kuiwakilisha Kaunti ya Mombasa.
“Nitawasilisha hoja ya kumng’oa Bw Ambani. Anamwangusha Gavana Nassir,” alisema Bw Katana, akiongeza kuwa siyo gavana anayewafeli wananchi bali maafisa aliowaamini.
Wawakilishi hao pia walimlaumu Ambani kwa kutopatikana kwa urahisi kwa njia ya simu na kuchelewesha utoaji wa fedha, jambo walilosema linaharibu sura ya serikali ya kaunti.
Hata hivyo, Bw Ambani alijitetea akisema tatizo lilikuwa ni ukosefu wa fedha.
Alifafanua kuwa idara yake ilitengewa Sh27 milioni pekee kwa mwaka mzima kushughulikia watoto, vijana, wanawake, na watu wenye mahitaji maalum — kiwango alichosema hakitoshi.