Wezi wavunja kanisa, waiba mali ya Sh300,000
MALI yenye thamani ya Sh300,000 iliibwa wezi walipovamia kanisa la Kianglikana la Kitharaini, Kaunti ya Kirinyaga.
Uvamizi huo uliotekelezwa Jumatatu usiku uliwastaajabisha waumini na viongozi wa kanisa hilo.
Waumini waliwashutumu wavamizi kwa kunajisi pahali patakatifu kwa kuvunja na kuiba mali iliyowekwa wakfu kumwabudu Mungu.
Mchungaji Susan Murimi, alisimulia jinsi alivyofika kanisani baada ya kudokezewa na kupata mlango ukiwa umevunjwa na baadhi ya vifaa kutoweka.
Vipaaza sauti vitatu, spika mbili na mtambo wa kusawazisha sauti ni miongoni mwa vifaa vilivyoibiwa.
“Kila mtu anahofu kuhusu wizi wa mali ya kanisa. Hatuna kitu cha kutumia kuhubiri na kumwimbia Mola Jumapili ijayo. Wezi walipotea hadi na kifaa cha kufunga mlango,” alisema.
Mwajiriwa wa kanisa hilo, Elizabeth Gatembu, alisimulia jinsi alivyofika kuosha kanisa kama kawaida yake, na kupigwa na butwaa alipokuta mlango wa kanisa ukiwa wazi.
“Nilijua majambazi wametumia nguvu kuingia kanisa nilipoona mlango umevunjwa. Nilifahamisha usimamizi wa kanisa ili waje kutathmini hali,” alisema.
Mweka hazina wa kanisa, Mwangi Wambiri, alisema suala hilo limeripotiwa katika Kituo cha Polisi cha Gathoge kwa uchunguzi.
“Tulifahamisha makachero waliozuru eneo hilo baadaye kufanya uchunguzi,” alisema Bw Wambiri.
Alisema majambazi wanaoaminika kutoka eneo hilo, sasa wanalenga sehemu takatifu.
Wapelelezi wameomba wakazi na waumini kushirikiana na kutoa habari muhimu za kutambulisha wahusika.