Willis Raburu ataka Sh10 milioni kutoka kampuni ya pombe
MWANAHABARI na mtayarishaji wa maudhui, Willis Raburu, amewasilisha kesi mahakamani akidai kampuni ya kutengeneza pombe ya East African Breweries Limited (EABL) kiasi cha Sh10 milioni kwa huduma alizotoa bila kulipwa.
Kupitia kampuni yake ya Steizon Limited, Raburu anaomba Mahakama Kuu kusimamisha leseni ya EABL hadi deni hilo lilipwe kikamilifu.
Katika kesi iliyowasilishwa chini ya cheti cha dharura, Raburu anadai EABL “imevunja haki zake na kumnyima mapato yake halali.”
Raburu anasema Game Changer Marketing Limited, kwa niaba ya EABL, ilimkabidhi jukumu la kufanya matangazo ya kampeni ya BebaBeba na huduma nyingine za kutangaza tamasha za Furaha City Festival zilizofanyika Desemba 7, 2024.
Baada ya kutekeleza kazi hiyo, Raburu anasema hakulipwa, hali iliyomuacha akidaiwa na wasanii na wataalamu alioajiri kufanikisha kampeni hiyo.
Kupitia wakili wake Danstan Omari, Raburu anasema hatua ya EABL kukataa kulipa Sh10 milioni “ni hujuma ya kiuchumi na inawadunisha watayarishaji wa maudhui, ambao ajira zao zinategemewa na maelfu ya vijana waliokamilisha vyuo.”
“Naomba mahakama itoe maagizo ya muda ili Raburu aweze kuwalipa wasanii waliofanikisha tamasha hilo mwaka jana,” Omari aliomba.