Wito makao makuu ya EAC yahamishwe kutoka Arusha hadi Kisumu
BUNGE la Wenye Nchi Homa Bay sasa linapendekeza makao makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) yahamishwe kutoka Arusha hadi Kisumu.
Walisema tukio la wiki jana ambapo mawakili na wanaharakati wa Kenya walizuiwa kuhudhuria kesi ya Kiongozi wa Upinzani Tanzania Tundu Lissu, linaonyesha kuwa hakuna demokrasia au heshima ya haki katika taifa hilo jirani.
Baadhi ya waliotimuliwa Tanzania ni Kiongozi wa PLP Martha Karua, Jaji Mkuu wa zamani Willy Mutunga, Mwanaharakati Bonface Mwangi na Mwanaharakati wa Uganda Agather Atuhaire ambaye alidai alibakwa wakati ambapo alikuwa akizuiwa.
Wanachama wa bunge la wenye nchi Homa Bay wanasema Kisumu inafahamika kutokana na kupigania haki na demokrasia kwa hivyo, itakuwa makao makuu mazuri kwa EAC.
Waliahidi kukusanya saini ili kuhakikisha kwamba makao makuu ya EAC yanahamishwa hadi Kenya. Arusha pia huwa ni mwenyeji wa Mahakama ya Afrika Mashariki, Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki na Mahakama kuhusu Haki Afrika.
Evance Otieno Oloo na Michaei Kojo ambao ni maafisa wa Bunge la Wenye Nchi walisema wamemwaandikia barua Waziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Beatrice Askul na kueleza nia yao ya kukusanya saini kuhamisha makao ya EAC hadi Kisumu.
“Sisi tunakusanya saini ili Kenya ijiondoe EAC au makao yake makuu yahamishwe hadi Kisumu,” ikasema sehemu ya ombi lao huku wakisema wanaharakati watakuwa na haki ya kujieleza jinsi wanavyotaka jijini Kisumu.
Mabw Oloo na Kojo pia walimtaka Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aombe msamaha kutokana na kauli yake kuwa wapiganaji wa haki Kenya na Uganda wamehamia kwake kuvuruga amani katika nchi hiyo.
Bw Oloo alisema ni wazi kuwa Bi Suluhu hajaonyesha juhudi zozote ya kuthamini sheria za EAC ambazo zimejikita katika haki, umoja na uwazi.