Wito Sakaja atekeleze ahadi alizotoa
BAADHI ya madiwani wa Kaunti ya Nairobi sasa wanamtaka Gavana Johnson Sakaja kuanza kutekeleza ahadi alizotoa kabla ya muda wa siku 60 aliyoomba kuisha.
Wakiongozwa na Naibu Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kaunti ya Nairobi, Bi Waithera Chege, ambaye pia ni diwani wa Wadi ya Nairobi South, madiwani hao walisema kuwa Gavana Sakaja aliahidi kushughulikia masuala muhimu yaliyowasilishwa katika bunge hilo.
Miongoni mwa masuala hayo ni utoaji wa fedha za karo (bursary) kwa wanafunzi wenye uhitaji, kuboresha miundombinu jijini, na kuongeza ufanisi wa huduma katika ngazi ya mashinani.
Hata hivyo, Bi Waithera alisema licha ya gavana kutoa hakikisho, ahadi nyingi bado hazijatekelezwa, hali inayowakatisha tamaa madiwani pamoja na wakazi wa Nairobi.
Alisisitiza kuwa masuala hayo ni nyeti kwa ustawi wa wakazi na kumtaka Gavana kuonyesha uwajibikaji na kutimiza ahadi alizotoa.
Wakati huo huo, Bi Waithera alimpongeza Rais William Ruto na Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kuingilia kati na kusuluhisha mvutano wa kisiasa uliokuwepo kati ya gavana na madiwani.
Alisema hatua hiyo imefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Bunge la Kaunti na Afisi ya Gavana, jambo ambalo ni muhimu ili kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kikamilifu Nairobi na Kenya kwa ujumla.
Diwani huyo alikuwa akizungumza wakati wa kugawa basari kwa wanafunzi 700 wanaotoka katika familia zisizojiweza.