Habari

Wito wa amani na uvumilivu wapamba Jumapili ya Mitende

April 14th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WAANDISHI WETU

WAUMINI wa Kanisa Katoliki nchini, Jumapili waliungana na mamilioni ya wenzao ulimwenguni kusherehekea Jumapili ya Mitende.

Sherehe hizo ambazo hufanywa Jumapili ya mwisho kabla ya Sikukuu ya Pasaka huadhimishwa kuashiria wakati ambapo Yesu aliingia Yerusalemu akiwa amebebwa na punda.

Jijini Nairobi, Kadinali John Njue aliongoza misa maalumu ya vijana katika Kanisa Katoliki la St Mary’s lililoko mtaani Lavington.

Alitoa wito kwa vijana wajitambue vyema ili kuepuka maovu yanayosababishwa na majaribu mengi wanayopitia ulimwenguni.

Katika kaunti ya Mombasa, viongozi wa kanisa Katoliki waliapa kupaza sauti na kukashifu vikali wanasiasa ambao wanatumia vibaya pesa za umma.

Msimamizi wa kanisa la Holy Ghost, Dayosisi ya Mombasa, Kasisi John Korea alisema kanisa ni sauti ya jamii na ufisadi unazuia maendeleo.

“Hatutakaa kimya, tutapaza sauti hadi wasikie kilio chetu hasa kuhusu ufisadi. Serikali inapaswa kukomesha ufisadi na wale ambao wameiba pesa za umma wapelekwe kortini ili wawe mfano kwa watu wengine wenye nia hiyo,” akasema.

Ujumbe wa kasisi Korea kwa wananchi wote ulikuwa kwamba waendelee kudumisha amani sherehe za Pasaka zinapokaribia.

Waumini walifurika kwenye barabara za mji wa Kisii, wakibeba matawi ya mitende kuadhimisha Jumapili ya Mitende ambayo pia ni mwanzo wa ‘Juma Takatifu’.

Padri Lawrence Nyaanga wa Chuo Kikuu cha Kisii aliwataka waumini kumwiga Yesu Kristo kwa vitendo vya unyenyekevu, mbali na kuwasaidia wasiojiweza.

“Kwa kuwasaidia wale wasiobahatika katika jamii, tutakuwa tunatimiza mapenzi ya Mungu,” akasema.

Padri huyo pia aliwaomba Wakenya kuombea amani nchini na kukashifu kitendo ambacho kilifanyika Mandera ambapo Madaktari wa Cuba walitekwa nyara na wanamgambo wa Al Shabaab.

Padri Nyaanga aliwaomba Wakenya kumwombea Rais Uhuru Kenyatta kupambana na ufisadi.

Aliwahimiza wanasiasa wote na viongozi wa kidini nchini kuhubiri amani, umoja na upatanisho ili nchi iimarike kiuchumi.

Katika Kaunti ya Nakuru, Askofu wa Dayosisi ya Nakuru Maurice Muhatia aliwaomba Wakristo kuwa na moyo wa subira na uvumilivu, hasa wakati huu ambapo changamoto za kimaisha zimeongezeka.

Mfano wa Yesu

“Tunawahimiza wakristo kote nchini kuwa wanyenyekevu kama Masihi, wakati akihudumu hapa duniani. Tuyanyooshe mapito yetu na kuombea taifa,” akasema.

Kwingineko katika eneo la Elburgon viungani mwa mji wa Nakuru, Askofu James Muraya aliwataka waumini kudumisha amani na upendo, akisema tangu uchaguzi uliopita ameshuhudia hali ya utulivu katika jukwaa la kisiasa.

Kulingana na tamaduni za waumini Wakatoliki, wao hulazimika kuhifadhi matawi ya mitende majumbani kwao kwa kipindi cha mwaka mmoja, wakisubiri Sikukuu ya Jumatano ya Majivu wakati ambapo mitende hiyo huteketezwa.

Ripoti za Diana Mutheu, Jadson Gichana, Amina Wako, Richard Maosi na Erick Matara