Habari

Wizara kuanzisha mpango wa kuufanya utoaji damu kuwa mazoea

September 11th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na MAGDALENE WANJA

WAZIRI wa Afya Sicily Kariuki amesema kuwa wizara yake itaanzisha mpango wa kufanya utoaji wa damu kuwa jambo la mara kwa mara ili kuahakikisha kuwa kuna viwango vya kutosha nchini.

Waziri Kariuki amesema hayo Jumatano alipozindua rasmi hafla ya wiki nzima ya utoaji damu iliyoandaliwa katika Makavazi ya Kitaifa jijini Nairobi.

“Tunayaomba mashirika ya serikali na yasiyo ya kiserikali pamoja na wananchi kulichukulia kama jukumu letu sote ili kuokoa maisha zaidi,” amesema waziri Kariuki.

Hafla hiyo imeandaliwa kutambua mchango wa Arjun Prasad Mainali ambaye ndiye bingwa wa kutoa damu dunia nzima.

Mainali ametoa damu wakati wa uzinduzi huo akifikisha mara 172 na kusalia bingwa ulimwenguni.

Kabla ya kuwasili nchini Jumanne, alikuwa ametoa damu mara 171.

 

Bingwa wa kutoa damu nchini Kenya Bw Alpha Kennedy Sanya akitoa hotuba yake Septemba 11, 2019. Picha/ Magdalene Wanja

Mainali amekuwa akizuru maeneo mbalimbali duniani katika kampeni za kuwahimiza watu kuhusu umuhimu wa kutoa damu.

Kulingana viwango vilivyowekwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), kipimo kimoja cha damu kinaweza kuokoa watu watatu na hivyo ameweza kuokoa maisha ya watu 513.

Mabingwa wawili wa utoaji damu wa hapa nchini ambao ni Bw Alpha Kennedy Sanya na Bi Aisha Dafalla wanatarajiwa kutoa damu katika siku ya mwisho ya hafla hiyo itakayokamilika Ijumaa.

Waziri wa Afya Sicily Kariuki (kati) amkabidhi zawadi Arjun Prasad Mainali (kushoto). Picha/ Magdalene Wanja