Wizara ya Usalama yalia bajeti kukatwa wakitaka pia pesa za kukarabati afisi
WIZARA ya Usalama wa Ndani inataka itengewe Sh15.44 bilioni katika mwaka ujao wa kifedha kufadhili matumizi ya siri, ukarabati wa Jumba la Harambee, safari za humu nchini za rais na ununuzi wa pikipiki kwa Maafisa wa Utawala wa Kitaifa (NGAO).
Hata hivyo, Wizara hiyo ilikosa kutengewa pesa hizo kulingana na Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) ya 2025 inayochambuliwa bungeni wakati huu.
Jumatatu, Katibu Msimamizi katika Idara ya Usalama Anne Ng’etich aliiambia Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Usalama kwamba kiasi hicho cha pesa ni muhimu katika kuiwezesha kutekeleza majukumu yake muhimu.
“Kutotengwa kwa pesa hizo (Sh15.44 bilioni) kutaathiri pakubwa utoaji huduma ikiwemo ushirikishi wa majukumu ya serikali ya kitaifa, kukamilishwa kwa miradi inayoendelea na kuendelezwa kwa operesheni za kiusalama zinazoendeshwa kote nchini,” akasewma Bi Ng’etich.
Fedha hizo zilikuwa sehemu ya Sh59 bilioni ambazo Wizara ya Usalama inataka itengewe katika mwaka ujao wa kifedha wa 2025/2026.
Kwa ujumla, wizara hiyo ilitaka itengewe Sh47 bilioni za kufadhili matumizi ya kawaida na Sh12 bilioni za miradi ya maendeleo.
Hata hivyo, Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS) imepunguza kiasi hicho hadi Sh37.52 bilioni, ambazo ni Sh30.5 bilioni za matumizi ya kawaida na Sh7 bilioni za maendeleo.
Akifafanua jinsi Sh15.44 bilioni walizoitisha na wakanyimwa, zingetumika, Bi Ng’etich alisema Sh1 bilioni zingeelekezwa kwa matumizi ya siri, zinazohusiana na usalama, Sh2.54 bilioni zikielekezwa katika kufanikisha ahadi ya Rais William Ruto ya kushirikisha wazee wa vijiji katika mfumo wa NGAO katika ngazi ya vijiji.
Kisha Sh2 bilioni zingetumika kununua jumla ya pikipiki 8000 kati ya 15,600 zinazohitaji, kuwawezesha machifu na wanaibu wao kusafiri haraka wanapowahudumia raia.
Nazo Sh200 milioni zilitarajiwa kutumika kukarabati jumba la Harambee House, ambayo ndio makao makuu ya Wizara ya Usalama wa Ndani.
“Sh749.5 milion na Sh274.7 milioni, mtawalia zingetumika kugharamia safari za rais za humu nchini na maandalizi ya sherehe za kitaifa” Bi Ngetich akaeleza.