Wizara yaagiza vituo vyote vya karantini katika shule vifungwe
JUMA NAMLOLA na FAITH NYAMAI
WIZARA ya Elimu imeiagiza ile ya Afya ifunge vituo vya karantini katika shule zote kufikia Jumatatu ijayo.
Kwenye barua kwa Katibu wa Wizara ya Afya, Bi Susan Mochache, Katibu anayesimamia elimu ya msingi Dkt Belio Kipsang anataka pia shule hizo zipigwe dawa kabla ya kurejeshwa kwa wizara yake.
“Kutokana na kuendelea kupungua kwa visa vya maambukizi, wadau katika sekta ya elimu wamependekeza shule zifunguliwe mapema kuliko tulivyokuwa tumekisia. Kwa sababu hiyo, tunaomba shule zote za umma zilizotumika kuwaweka wagonjwa wa corona mzipige dawa na kuturejeshea kufikia Septemba 28,” ilisema barua hiyo.
Dkt Kipsang alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na kwamba walimu watatakiwa warejee katika shule zao kwa maandalizi ya ufunguzi.
Naye Afisa Mkuu wa Tume ya Huduma za Walimu (TSC), Bi Nancy Macharia, amewataka wakuu wa elimu katika kaunti wahakikishe walimu wote wanarejea shuleni kufikia Jumatatu ijayo.
“Baada ya mashauriano na wadau wa sekta ya elimu, walimu wote walioajiriwa na TSC wanatakiwa warejee shuleni Septemba 28 ili kufanya maandalizi ya kufunguliwa kwa shule,” akaandika Bi Macharia.
Kati ya mambo wanayotakiwa kufanya shuleni ni kusimamia usafi kama kufyeka nyasi, kusafisha madarasa na kuweka mipango ya kutekeleza kanuni za usafi kuhusiana na maradhi ya Covid-19.
Kulingana na ripoti ya mwisho aliyokabidhiwa Waziri wa Elimu, Profesa George Magoha, shule zinatarajiwa kufunguliwa kati ya Oktoba 5 na 19.
Kwenye mapendekezo hayo, wanafunzi wa darasa la Nane na wale wa kidato cha Nne watakuwa wa kwanza kufungua ili wajiandae kwa mtihani wa mwisho ambao unapendekezwa ufanywe Aprili mwaka ujao.
Kurejea kwa wanafunzi hao kunalenga kuwapa nafasi walimu kujifunza kutekeleza kanuni za kudhibiti corona wakiwa na watoto wachache.
Wengine wanaotarajiwa kuwasili shuleni siku ya kwanza ni wanafunzi wa Darasa la Saba na wale wa Kidato cha Tatu.
Wanafunzi waliosalia watatarajiwa kuripoti shuleni wiki moja au mbili baada ya kundi la kwanza.