Wizara yapendezwa na jinsi Mombasa inavyokabili Covid-19
Na SAMMY WAWERU
WIZARA ya Afya imependezwa na jinsi ambavyo wakazi wa Mombasa wametilia maanani kanuni na mikakati iliyowekwa kuzuia kuenea kwa Covid-19.
Visa vya maambukizi vilivyoandikishwa Kaunti ya Mombasa vinaonekana kushuka katika kipindi cha wiki kadhaa sasa ikilinganishwa na idadi iliyokuwa ikiandikishwa siku za mwanzo Kenya ilipokuwa imethibitisha kisa cha kwanza.
Waziri Msaidizi katika Wizara, Dkt Rashid Aman mnamo Jumanne amesema mikakati iliyowekwa kusaidia kudhibiti maambukizi zaidi katika kaunti hiyo imeoenakana kuzaa matunda.
“Kila kaunti ina hali yake ya maambukizi ambapo baadhi zitapanda kama vile Kiambu na zingine kushuka kama vile Mombasa. Tumeridhishwa na Mombasa,” waziri Aman akasema.
Awali, Mombasa ndiyo ilichukua nafasi ya pili katika ongezeko la visa vya maambukizi ya corona nchini, nafasi ambayo sasa imetwaliwa na Kaunti ya Kiambu, ambayo katika wiki za hivi karibuni imekuwa ikiandikisha idadi ya juu.
Nairobi ndiyo inaongoza, ikifuatwa na Kiambu.
Dkt Aman hata hivyo, amesema vipimo vya Covid-19 vinaendelea kufanywa Mombasa.
“Tumeona visa Mombasa vikishuka, na ni ishara mikakati tuliyoweka kusaidia kuzuia maambukizi zaidi inazaa matunda,” akaelezea.
Kenya imethibitisha visa vipya 271 kutokana na sampuli 4,091 idadi jumla ikifika wagonjwa 30,636 kuwahi kuthibitishwa nchini.
Waliofariki kipindi cha saa 24 zilizopita ni watano idadi jumla ya wahanga Kenya ikifika watu 487.