Yabainika Al-Shabaab waliua wanajeshi 3 Lamu baada ya jaribio la kuvamia GSU kutibuliwa
IMEBAINIKA uvamizi na mauaji ya maafisa watatu wa Jeshi la Kenya (KDF) katika eneo la Badaa, kwenye barabara ya Kiunga-Sankuri, Lamu, Jumanne ulitekelezwa masaa machache baada ya jaribio la Al-Shabaab kushambulia kambi ya polisi wa kukabiliana na ghasia (GSU) kutibuliwa.
Uchunguzi wa Taifa Leo ulitambua kuwa magaidi wa Al-Shabaab waliojihami kwa silaha hatari awali walikuwa wamevamia kambi ya GSU ya Milimani, takriban kilomita 80 kutoka Badaa Jumapili jioni.
Pia walijaribu kuingia kwa lazima kijijini humo ili kuwadhuru wakazi lakini wakakabiliwa vilivyo na walinda usalama na kushindwa nguvu, hivyo kutokomea ndani ya msitu wa Boni.
Shambulio hilo lilitekelezwa majira ya saa kumi na mbili unusu jioni hiyo ya Jumapili, Julai 13,2025.
“Inasikitisha kwamba baada ya kukabiliana na kuwashinda nguvu Al-Shabaab wakati wakijaribu kuvamia kambi ya GSU Milimani Jumapili, walikaa siku mbili na kisha kutekeleza shambulio na mauaji ya KDF wetu watatu na kujeruhi wengine sita eneo la Badaa Jumanne,” akasema mmoja wa walinda usalama aliyedinda kutajwa jina.
Siku hiyo ya Jumanne asubuhi, wakazi wa kijiji cha Milimani walizongwa na wasiwasi pale mashine ya kurushia guruneti kwa mbali (RPG) ilipogunduliwa kwenye manyasi na wanafunzi waliokuwa wakielekea shuleni papo hapo kijijini Milimani.
Kijiji hicho ni makazi ya Zaidi ya watu 350 wote wakiwa ni kutoka jamii ya walio wachache ya Waboni.
Guruneti hiyo inaaminika kudondoshwa na Al-Shabaab waliokuwa wakitorokea usalama wao msituni Jumapili punde waliposhindwa nguvu na walinda usalama Milimani.
Kamishna wa Kaunti ya Lamu, Bw Wesley Koech alithibitisha kutekelezwa kwa jaribio hilo la uvamizi wa kambi ya GSU na kijiji cha Milimani Jumapili.
Pia alithibitisha kuonekana kwa RPG hiyo ikiwa imeangushwa kijijini.
Alisema maafisa wa usalama walitumwa eneo husika na kutathmini hali kabla ya kuiondoshwa kwa kuiharibu RPG hiyo.
“Ni kweli. Kulikuwa na jaribio la Al-Shabaab kuvamia kijiji cha Milimani na kambi ya GSU iliyoko karibu na kijiji hicho. Jaribio lao lilitibuliwa kwani maafisa wetu walikuwa macho kuwakabili kwa ujasiri na kuwashinda maadui hao. Kuhusu RPG, ni kweli kifaa hicho kilionekana Milimani. Tulituma maafisa wetu kule na tayari kifaa kimeondolewa. Watu wasiwe na shaka. Ulinzi umeimarishwa kote,” akasema Bw Koech.
Akigusia mauaji ya wanajeshi watatu wa KDF na wengine sita waliojeruhiwa, Bw Koech alitoa pole kwa wahusika huku akiwasihi raia kutoa taarifa zitakazosaidia kukabiliana na kumwangamiza adui.
“Ningesihi tuwe na ushirikiano. Wananchi watupe taarifa sisi kama walinda usalama ili kusaidia kukabiliana na wahalifu na Lamu iendelee kuwa na amani,” akasema Bw Koech.
Shambulizi lililoacha KDF watatu wakiuawa na sita kujeruhiwa linajiri wakati ambapo operesheni ya usalama kwa jina Amani Boni inaendelezwa na serikali kuu ndani ya msitu wa Boni.
Operesheni hiyo ilizinduliwa Septemba 2015, dhamira kuu ikiwa ni kuwasaka na kuwamaliza au kuwafurusha magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo mkuu wa Boni.
Tangu operesheni kuzinduliwa imeshuhudia kupungua kwa visa vilivyoshuhudiwa kila mara vya Al-Shabaab kuua raia na walinda usalama.