Yafaa Badi ajumuishwe katika baraza la mawaziri?
Na CHARLES WASONGA
HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta kumjumuisha Mkurugenzi Mkuu wa Kitengo cha Huduma za Nairobi (NMS) Mohammed Badi katika baraza la mawaziri imeibua hisia mseto miongoni mwa viongozi na wataalamu ya masuala ya sheria na Katiba.
Baadhi yao walitaja hatua hiyo kama inayokwenda kinyume na Katiba na kutoa mfano mbaya katika utawala wa kisheria. Na wengine waliunga mkono wakisema Rais hakukiuka Katiba wala kuvunja sheria yoyote.
Meja Jenerali Badi alilishwa kiapo cha kuweka siri Alhamisi, Septemba 10, 2020, katika Ikulu ya Nairobi na hivyo kuruhusiwa kuhudhuria mikutano ya baraza la mawaziri na kamati zake zote. Ikulu ilisema Rais Kenyatta alichukua hatua hiyo kulinga na Agizo Kuu Nambari 3 ya 2020, alilotoa mwezi Juni mwaka huu.
Meja Badi aliapishwa katika hafla fupi iliyoongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua katika Ikulu ya Nairobi na kushuhudiwa na Rais Kenyatta mwenyewe.
Hatua hiyo ni ya hivi punde ambayo Rais Kenyatta amechukua kupiga jeki kazi ya NMS huku Gavana wa Nairobi Mike Sonko akilalamika kuwa idara hiyo imetwaa majukumu zaidi yale manne ambayo walikubaliana hasimamiwe na Serikali ya Kitaifa.
Kufuatia kujumuishwa katika baraza la mawaziri Meja Jenerali Badi alihudhuria vikao vya Kamati ya Baraza la Mawaziri Kuhusu Utekelezaji wa Mipango ya Serikali ya Kitaifa, ambayo mwenyekiti wake ni Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i.
Badi huwajibika moja kwa moja kwa Rais Kenyatta kwa sababu Idara ya NMS iliwekwe chini ya Afisi ya Rais kufuatia Agizo Kuu la mwezi Juni, 2020. Yeye ni miongoni mwa maafisa 12 wa kijeshi ambao waliopewa nafasi ya kusimamia asasi za kiraia ili kupiga jeki utendakazi wazo.
Mtaalamu wa Masuala ya Kikatiba Bobby Mkangi alisema japo watu wengine wanaweza kushirikishwa katika baraza la mawaziri, uteuzi wa Badi unaweza kuashiria kupanuliwa kwa idadi ya mawaziri kuzidi 22 inayokubalika kikatiba.
Mkangi ambaye alikuwa mwanachama wa Kamati ya Wataalamu walioandika Katiba 2010 (CoE) alisema hatua ya Rais Kenyatta huenda ililenga kusuluhisha kosa fulani kwamba kumekuwepo na masuala kuhusu uhalali wa NMS.
“Kumekuwepo na madai kuwa NMS ni asasi ambayo haitambuliwi kikatiba. Kuna wale ambao walikuwa wakihoji ikiwa imepewa sifa ya Shirika la Serikali Kuu. Huenda Rais alitaka kuiweka mahala fulani katika Afisi ya Mawaziri. Hii inaibua maswali kuhusu hadhi ya Nairobi hasa baada ya kuhamishwa kwa majukumu manne makuu hadi Serikali Kuu,” akasema Bw Mkangi.
Lakini anaongeza kuwa, kisheria, Kaunti ya Nairobi inafaa kuwa huru kiusimamizi.
Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria Nchini (LSK) Nelson Havi anasema mtu yeyote ambaye sio waziri au amepewa idhini kikatiba kuketi katika baraza la mawaziri, hawezi kufanya hivyo.
“Hata kama Rais atamteua mtu, sharti mtu huyo apigwe msasa na bunge ndiposa aweze kuteuliwa rasmi kutekeleza majukumu ya uwaziri. Kwa hivyo, Badi hawezi kuketi katika baraza la mawaziri. Badi ni afisa wa kijeshi; afisa kama huyo hawezi kuteuliwa waziri. Sharti ajiuzulu kwanza,” akasema Bw Havi.
Kauli ya mwenyekiti huyo wa LSK inaungwa mkono na mawakili Steve Ogola na James Mwamu.
Bw Mwamu anaseama kile ambacho Rais Kenyatta alifanya ni kupanua muundo wa Serikali Kuu na ile ya Kaunti kwa kupanua baraza la mawaziri na kutwaa majukumu manne makuu ya serikali ya kaunti ya Nairobi.
“Hii ni serikali ya kiraia. Uteuzi wa Meja Badi kuwa waziri ni kinyume cha Katiba. MNS ilikuwa ni asasi ya muda iliyobuniwa kusimamia utekelezaji wa majukumu manne yaliyohamishwa hadi Serikali ya Kitaifa. Hii sio asasi ya Kikatiba. Kupanua serikali kukidhi masilahi ya kisiasa hakuruhusiwi,” akasema Wakili Ogolla.
Wakili Mwamu anasema masilahi ya NMS yangewakilishwa katika baraza la mawaziri na Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa ambaye alikuwepo wakati wa kutiwa saini kwa mkataba wa kuhamisha majukumu kutoka serikali ya Nairobi hadi Serikali kuu. Halfla hiyo ilifanyika katika Ikulu ya Nairobi mnamo Februari 15, 2020, na kushuhudiwa na Rais Kenyatta na Spika wa Seneti Kenneth Lusaka.
Lakini Wakili wa Serikali Ken Ogeto anatetea hatua hiyo akisema kuwa Rais Kenyatta hakukiuka Katiba wala sheria yoyote kwa kumjumuisha Meja Badi katika Baraza la Mawaziri.
“Sheria inampa Rais idhini ya kumwalika mtu yeyote katika baraza la mawaziri kusaidia hapa na pale,” akasema bila kutaja sheria hiyo.
“Badi sio Waziri. Hapa mimi ninaweza kuhudhuria vikao vya baraza la mawaziri nikialikwa. Hatua hiyo sio kinyume cha sheria,” Ogeto akasema.
Aliongeza kuwa NMS iliwekwa chini ya Afisi ya Rais, hatua ambayo inampa Rais nafasi ya kumshirikisha Badi katika baraza la mawaziri.
“Nani alisema mwanajeshi hawezi kuhudhuria mikutano kama hiyo. Yeye ni Mkenya, na Rais anaruhusiwa kumwalika mtu yeyote katika baraza la mawaziri mradi alishwe kiapo cha kuweka siri,” Bw Ogeto akaeleza.