Yafichuka Uhuru alimtuma Ruto kwa Munya
Na VALENTINE OBARA
UAMUZI wa Rais Uhuru Kenyatta kutohudhuria kongamano la kibiashara katika jumba la KICC jijini Nairobi, ndio ulimpelekea Naibu Rais William Ruto kukaa sako kwa bako na Waziri wa Biashara na Viwanda, Bw Peter Munya, ambaye ni miongoni mwa waliodaiwa kupanga njama ya kumuua.
Imefichuka Rais Kenyatta ndiye alipaswa kufungua rasmi kongamano hilo la siku mbili ambalo mgeni mwengine mkuu alikuwa ni Kiongozi wa Chama cha ODM Raila Odinga, aliye hasimu mkubwa wa kisiasa wa Dkt Ruto.
Bw Odinga alisema alihudhuria kama balozi wa miundomsingi katika Muungano wa Afrika (AU).
Bw Munya ambaye ndiye alikuwa kiongozi wa hafla, alisema Rais alikuwa na majukumu mengine ndipo akamtuma naibu wake kumwakilisha haflani.
“Naibu Rais atafafanua kwamba Rais alifaa kuwa hapa lakini kutokana na majukumu mengine ya dharura na pia kwa vile atakuwa hapa Jumatano pamoja na wakuu wengine wa mataifa ya kigeni, aliomba tumruhusu asihudhurie leo,” akasema Bw Munya.
Wakati aliposimama kuhutubu, Dkt Ruto alitilia mkazo matamshi hayo na kuongeza kwamba Rais atakuwa KICC leo kufungua rasmi kongamano la kibiashara la COMESA, ambalo linatarajiwa kuhudhuriwa pia na wakuu wa mataifa ya nje.
Uhusiano kati ya Bw Munya na Dkt Ruto haujakuwa mzuri tangu ilipodaiwa waziri huyo ni miongoni mwa wengine waliopanga njama ya kumuua naibu rais walipokutana kisiri katika hoteli ya La Mada jijini Nairobi.
Hii ilikuwa mara yao ya kwanza kuonekana wakiwa karibu hadharani tangu madai hayo yanayotishia kugawanya Baraza la Mawaziri kuibuka mwezi uliopita.
Ilisemekana Naibu Rais ndiye alipiga ripoti kwa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) akihofia maisha yake baada ya barua kusambazwa mtandaoni ikidaiwa iliandikwa na waziri mmoja kwa Rais Kenyatta.
Barua hiyo ilionyesha waziri ambaye jina lake lilifichwa, akilalamikia jinsi alivyolazimishwa kuhudhuria mikutano ya kisiri ya kupanga maovu dhidi ya Dkt Ruto.
Afisa wa Mawasiliano Kidijitali katika Ikulu, Bw Dennis Itumbi alifikishwa mahakamani kushtakiwa kwa madai ya kusambaza barua hiyo inayoaminika kuwa feki kwa wanasiasa wa kikundi cha Tanga tanga, ambao pia wanachunguzwa.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na wawekezaji pamoja na wadau wengine wa kibiashara, na Dkt Ruto alitilia mkazo hitaji la wafanyabiashara kuongeza bidhaa wanazouza nje ya nchi.
“Ni wazi kwamba kiwango cha bidhaa za Kenya zinazouzwa nje ya nchi ni kidogo ikilinganishwa na uwezo wetu katika ukanda huu na soko la ulimwenguni,” akasema.
Rais Kenyatta alikuwa amehudhuria kongamano lingine katika Taasisi ya Mafunzo ya Fedha ya Kenya (KSMS) iliyo eneo la Ruaraka, Nairobi.
Kongamano hilo lilihusu masuala ya teknolojia za kifedha, ambapo Rais alisema Kenya itaendelea kutumia teknolojia za kisasa kurahisisha utoaji huduma za kifedha kwa umma.
Katika hotuba yake, Bw Odinga alitaja masuala kama vile ufisadi, urasimu na uchochezi wa kisiasa kama changamoto kuu zinazotatiza biashara kati ya mataifa ya bara hili.
Alikashifu Tume ya Kudhibiti Kawi na Petroli kwa kuhangaisha waekezaji wanaotaka kufanya biashara ya kuzalisha kawi nchini, ambayo ni rasilimali muhimu ya kuvutia uwekezaji wa kiviwanda.