Habari

Zawadi hewa kutoka China

August 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI imethibitisha kuwa kontena ambayo ilitarajiwa kwamba ilisheheni bidhaa za kieletroniki zilizotolewa kwa bunge kama zawadi kutoka China haikuwa na chochote ilipowasili nchini.

Kulingana na stakabadhi za usafirishaji, kontena hiyo ilitarajiwa kubeba vipakatalishi 46, projekta tano na kamera nne ambazo zilikuwa zimetolewa na chama cha National People’s Congress (NPC) cha China kama zawadi.

Kwa hivyo, Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) haitafanya uchunguzi kuhusu tukio hilo la kushangaza, na badala yake serikali imeitaka China kuchunguza suala hilo.

China imetakiwa kutumia maafisa wa ubalozi wake kuchunguza jinsi konteina halisi ambayo ilipasa kuletwa nchini ilitoweka.

Uamuzi huo ulifikiwa Alhamisi kwenye mkutano uliofanywa katika majengo ya Bunge na kuhudhuriwa na maafisa wa usalama na wawakilishi wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) na Mamlaka ya Bandari Nchini (KRA).

Maafisa hao walikagua stakabadhi husika za kupitisha bidhaa bandarini pamoja na picha za konteina hiyo, zilizoonyesha wazi kwamba ilikuwa tupu. “Tumeamua kwamba Ubalozi wa China ufuatilie suala hilo na maafisa wao kule China kubaini kilichopelekea kusafirishwa kwa konteina tupu badala ya ile iliyosheheni bidhaa za kieletroniki,” akasema Karani wa Bunge la Kitaifa Michael Siala kwenye taarifa kwa vyombo vya habari.

Kawaida mizigo ya ubalozi huwa haikaguliwi inapofungwa na wanaohusika kwenye bandari inakotumwa. Kinachoangaliwa huwa ni fomu maalum ya kibalozi, inayoonyesha ni bidhaa gani zinazosafirishwa na zinamwendea nani. Bw Sialai alisema maafisa wa ubalozi wa China walifika bungeni Alhamisi na kufahamishwa kuhusu suala hilo na “makubaliano yakaafikiwa kuwa wachunguze utata kuhusu zawadi hiyo nchini China.”

“Ni kweli kwamba konteina hiyo iliwasilishwa katika uwanja wa bunge mnamo Julai, 2019, niliwaagiza maafisa wa bunge la kitaifa kuthibitisha kupokelewa kwa bidhaa zilizoorodheshwa katika stakabadhi tuliyopokea kutoka ubalozi wa China.

Tupu

Bw Sialai alisema vibandiko vya kontena hiyo vilipokatwa na ikafunguliwa, ilipatikana kuwa tupu.

“Maajenti wa ubalozi wa China na maafisa wetu walinifahamisha kuhusu suala hilo na nikaamua kwamba, maafisa wa DCI walioko katika kituo cha Polisi cha Parliament Road wajulishwe.

Polisi walisema konteina hiyo ilichunguzwa ilipowasilishwa katika depo za makonteina eneo la Embakasi na ilionekana kuwa tupu. Baada ya hapo, maajenti wa kupitisha bidhaa waliwasiliana na maafisa wa ubalozi na wenzao nchini China kuthibitisha ukweli kuhusu maelezo yaliyomo kwenye konteina hiyo.

Kwa upande wake, ubalozi wa China jijini Nairobi ulisema unaamini kuwa suala hilo litatatuliwa na bidhaa zilizotoweka kurejeshwa.

“Kwa miaka mingi, Wachina wamekuwa wakitoa zawadi kwa ndugu na dada zetu wa Kenya, kama vile vifaa vya kimatibabu, vifaa vya afisi na misaada ya chakula, ambayo imekuwa ikiwasilishwa salama. Miongoni mwa bidhaa hizo ni vifaa vya kiafisi vilivyowasilishwa kwa Bunge la Kitaifa mnamo 2018. Kwa hivyo, hii ni mara ya kwanza kwa tukio kama hili kutokea,” ikasema taarifa kutoka ubalozi wa China.