Habari

Ziara ya Abagusii Ikulu ilikuwa njama ya kumkata mbawa Matiang’i – Vijana

Na WYCLIFFE NYABERI August 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KUNDI la vijana walio na taaluma mbali mbali na viongozi chipukizi kutoka eneo la Gusii wamesema “jamii ya Abagusii haitapigwa mnada” kufuatia ziara ya hivi majuzi katika Ikulu ya Nairobi.

Ijumaa wiki jana, viongozi waliochaguliwa kutoka Gusii ambao ni washirika wa karibu katika utawala wa Kenya Kwanza waliongoza ujumbe wa zaidi ya watu 5,000 kutoka kaunti za Kisii na Nyamira hadi Ikulu ya Nairobi kwa mkutano na Rais Ruto.

Wapangaji wa mkutano huo wakiongozwa na Mbunge wa Mugirango Kusini na kinara wa walio wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro, walidokeza kuwa lengo la ziara hiyo lilikuwa ni kufanya mazungumzo na rais kuhusu maeneo muhimu ya maendeleo ambayo jamii ya Gusii inayataka.

Bw Osoro pamoja na wenzake Zaheer Jhanda (Nyaribari Chache), Japheth Nyakundi (Kitutu chache Kaskazini), Alfa Miruka (Bomachoge Chache) Dorice Aburi (Mwakilishi wa Kike wa Kisii), Steven Mogaka (Mugirango Magharibi), Jerusha Momanyi (Mwakilishi wa Kike wa Nyamira) na Irene Mayaka (mteule) walitaja safari hiyo kuwa yenye ufanisi tele.

Lakini wakizungumza mjini Kisii, saa 24 tu baada ya ziara ya Nairobi, vijana hao walidai kuwa hatua hiyo ililenga kuibua hisia za jamii ya Gusii kwamba Rais William Ruto ana maslahi yao moyoni ilhali amewapuuza.

Pia kundi hilo liliongeza kuwa hiyo ni hatua iliyopangwa vyema, inayolenga kukatisha hamu ya jamii ya Abagusii kumuunga mkono mwanao- aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i ambaye ametangaza nia yake ya kumenyana na Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

Vijana hao walishutumu waliopanga ziara hiyo ka kuwataja kama watu wenye ubinafsi mwingi na kujipiga kifua. Waliitaka jamii ya Abagusii kusalia na umoja katika kumuunga mkono Dkt Matiang’i.

Walimkaripia rais kwa kutotekeleza miradi mingi ambayo aliahidi eneo hilo miaka michache iliyopita na kushangaa jinsi ahadi hizo zitawezekana wakati huu.

“Ni mwaka mmoja tu kabla ya sisi kuingia katika kipindi cha kampeni na umewapeleka watu wetu hadi Ikulu kuwaambia kwamba utakamilisha miradi yote uliyoahidi. Kwa nini hukuikamilisha kwa muda uliopangwa? Ni kwa sababu umehofia wa ushawishi unaoongezeka wa mtoto wetu Dkt Fred Matiang’i,” Elijah Bogita, kiongozi wa vijana kutoka Nyaribari alisema akimrejelea rais.

Aliongeza kuwa Wakenya sasa wamekomaa na hawapigi kura kamwe kwa mtu anayewapa hela chache ndiposa wampigie kura.

Bw Bogita alinyooshea kidole cha lawama wabunge wa Kenya Kwanza kutoka eneo la Gusii kwa kufanya kidogo kuchochea maendeleo kwa watu wao. Aliwataka wajifunze kutoka kwa wenzao wa Luo Nyanza.

“Nataka kuwaambia viongozi wetu, angalieni wenzanu wa Luo Nyanza wanafanya nini. Hawapeleki watu wao katika ikulu ya serikali bure. Tazama tulivyoona juzi huko Homabay wakati wa Kongamano la Ugatuzi. Barabara bora, miundomsingi bora na vingine vingi. Hili ndilo tunalotaka kwa watu wetu lakini si kuwapa pesa kidogo na kuwataka wapige makofi kutwa nzima,” Bw Bogita aliongeza.

Vijana hao waliwatahadharisha viongozi wote waliochaguliwa Gusii na wanampinga Dkt Matiang’i kuwa watakabiliwa na kibarua cha kutetea viti vyao 2027.

“Wacha niwahakikishie, kiongozi yeyote kutoka eneo hili, ambaye atakuwa kinyume na mgombeaji wetu Dkt Fred Matiang’i atachukuliwa kuwa adui wa jamii. Itakuwa kama mwaka wa 2002 ambapo marehemu Simeon Nyachae aliwania urais . Wale wote waliokuwa dhidi yake waliadhibiwa kwenye kura na taluma zao za kisiasa zikazikwa hadi wa sasa,” alisema kijana mwingine Denis Mosoti.

Seneta wa Nyamira Okong’o Omogeni pia aliunga mkono sauti za vijana hao katika kukashifu ziara ya Ikulu na kuwataka waliopewa pesa hizo kuzitafuna lakini kufanya maamuzi ya busara katika uchaguzi ujao.

“Wacha niwaambie watu wangu. Chukua pesa hizo mlizopewa lakini kumbuka kama jamii, tuko nyuma ya mtoto wetu Dkt Fred Matiang’i. Lazima tuendelee kumuunga mkono na kumuombea,” seneta Omogeni alisema na kuwataka wapiga kura kuwaadhibu wale ambao watakuwa kinyume na Dkt Matiang’i.

Kulingana na mwakilishi wa kike wa Kisii Donya Dorice Aburi, ambaye alikuwa sehemu ya viongozi walioongoza ujumbe huo hadi Ikulu, Rais Ruto aliwaahidi wakazi wa Gusii kikapu kizima.

Mbunge huyo alisema rais aliahidi kukamilisha miradi yote iliyokwama kama vile barabara, kituo cha saratani na ujenzi wa haraka wa Chuo Kikuu cha Nyamira.

Rais pia anasemekana kubadili nia yake ya hapo awali ya kutaka kuuhamisha uwanja mdogo wa ndege wa Suneka kuhali kwingine.

Pia, kiongozi wa taifa aliahidi makuu kwa kuboresha uwanja wa Gusii na kuipa klabu ya soka ya Shabana basi jipya. Rais Ruto pia aliahidi upanuzi wa barabara ya Bomet-Kaplong-Chepilat-Kisii, ujenzi wa masoko ya kisasa, nyumba zaidi miongoni mwa mengine.