HabariSiasa

ZIARA YA MAY: Fedha zote za ufisadi zilizofichwa Uingereza kurejeshwa nchini

August 30th, 2018 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

KENYA na Uingereza Alhamisi zilitia saini mkataba ambao utahakikisha kuwa pesa na mali nyingine zilizoibwa na kufichwa huko Uingereza zinarejeshwa, katika juhudi za Rais Uhuru Kenyatta za kupambana na ufisadi.

Mkataba huo uliafikiwa wakati wa mkutano kati ya Rais Kenyatta na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, ambaye alizuru Kenya kwa ziara ya siku moja, miaka 30 tangu aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo Margaret Thatcher azuru taifa hili.

Huu ulikuwa mkataba wa pili wa aina hiyo katika kipindi cha miezi mitatu baada ya Kenya kutia mwingine na Uswizi Juni mwaka huu wakati Rais wa Uswizi Alain Berset alitembea katika Ikulu ya Nairobi.

Katika hotuba yake, Rais Kenyatta alisifu mkataba huo wa Kenya na Uingereza akisema utasaidia kuzuia ufisadi.

“Tunafaa kuifanya kuwa uchungu kwa kutowafaidi wanaojihusisha na ufisadi, na iwe ghali ili waepuke,” akasema katika ikulu ya Nairobi.

Japo hakusema kiwango cha mali na pesa zinazotarajiwa kurejeshwa kutoka UK, Rais Kenyatta alisema hiyo itasaidia katika vita dhidi ya ufisadi.

Bi May naye alisema Uingereza itaanzisha mradi wa kusaidia wanajeshi wa Amisom walioko Somalia ili kuimarisha juhudi za kukuza amani.

Aidha, Bi May alisema wanajeshi wa Kenya wataanza kufanya mazoezi ya pamoja na wale wa UK, ambayo yatahusisha kuhusu ujuzi wa kukabiliana na vilipuzi vya kutegwa ambavyo hutumiwa na magaidi.

“UK ndilo taifa kubwa zaidi kutoka nje ambalo limewekeza Kenya na ni lengo letu kuwa taifa la G7 lililowekeza zaidi Afrika kufikia 2022,” Bi May akasema.

“Tunapojipanga kuondoka EU tumejitolea kuondoka vyema na kuendeleza ushirikiano wetu wa kibiashara.”

Kenya ilinunua bidhaa zinazogharimu Sh38.55 bilioni kutoka Uingereza mwaka wa 2017, likiwa ndilo taifa lilioongoza kwa biashara  barani Uropa.