Zogo latokota serikali jumuishi wandani wa Rais wakidai baadhi ODM wamejaa ulafi
MIPASUKO imetokea katika ushirikiano wa UDA na ODM huku wandani wa Rais William Ruto wakiwashutumu baadhi ya viongozi wa ODM kwa kumsukuma kiongozi wa nchi ili wanufaike ndani ya serikali jumuishi.
Kilichozua shutuma hizo ni hatua ya Gavana wa Kisumu Profesa Anyang’ Nyong’o mnamo Jumanne, kudai kwamba serikali ya Rais Ruto inalenga kurejesha Kenya nyuma wakati ambapo mfumo wa ugatuzi haukuwa umekumbatiwa.
Gavana huyo alikerwa na hatua ya serikali kukataa kuachia kaunti zisimamie fedha za ujenzi wa barabara, akisema kaunti zimekuwa zikisimamia vyema sekta ya afya ambayo ililemea serikali kuu.
Alisema serikali kuu haingeweza kusimamia Hospitali Kuu ya Kenyatta ambayo ilibakia chini ya usimamizi wake ilhali inakazia kaunti pesa za ujenzi wa barabara mashinani.
Prof Nyongó mmoja wa viongozi waliopigania mfumo wa vyama vingi nchini, alisema kuwa kuna kibarua kuhakikisha ugatuzi unatekelezwa kikamilifu chini ya utawala wa sasa.
“Ufanisi ambao ulipatikana wakati wa ukombozi wa pili nchini hatuwezi kukubali uharibiwe na utawala huu,” akasema Prof Nyongó.
Jana, Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Seneti, Bw Aaron Cheruiyot, alimchemkia Prof Nyongó na baadhi ya wanasiasa wa ODM, akisema wanania ya kumfumba macho Rais hasa kuhusu utekelezaji wa makubaliano kati ya pande zote mbili.
“Ni vigumu sana kuwa William Samoei Ruto. Wabunge wa ODM kama tu wenzao wanalenga kusalia na hazina ya kusimamia ujenzi wa barabara,” akasema Bw Cheruiyot.
“Seneti iliunga mkono magavana kuhusu hili ili wachukue usimamizi wa hazina hii lakini haikufanikiwa. Inashangaza sasa Profesa Anyang’ Nyongó analaumu Rais kwa suala hilo. Huku ni kumfumba macho kiongozi wa nchi,” akasema Bw Cheruiyot.
Hata hivyo, alijibiwa vikali na Seneta wa Nairobi, Bw Edwin Sifuna, akisema hana mamlaka ya kuingilia na kuwashambulia viongozi wa ODM kuhusu suala lolote la kitaifa.
“Raila mwenyewe amezungumza hadharani kuhusu suala hili na kutoa maoni yake lakini bado hatujamsikia kiongozi wa UDA,” akasema Bw Sifuna.
“Namkumbuka Kiongozi wa wachache Junet Mohamed akisema tutafuata mwelekeo wa Raila kuhusu suala hili lakini bado sijamsikia Kiongozi wa Wengi Kimani Ichung’wah,” akaongeza.
Mbunge mmoja wa UDA, alisema sasa ODM imepita mpaka kwa sababu sasa inatumia ushirikiano huo kumfumba macho rais ikitumia katiba ili kutimiza maslahi yao.
“Rais aliingia kwenye ushirikiano na ODM kwa roho safi lakini sasa baadhi ya viongozi hao wanatumia hilo kumpiga vita ili aridhie matakwa yao kuhusu kila kitu,” akasema mbunge huyo ambaye hakutaka jina lake linukuliwe.
Naibu Kiongozi wa ODM, Bw Godfrey Osotsi pia ameshutumu utawala wa Rais Ruto kwa kupuuza utekelezaji wa yaliyomo kwenye mkataba kati ya mirengo yote miwili.
“Tulitia saini mkataba huo ili kutoa kipaumbele kwa suluhu kuhusu masuala yaliyoibuliwa wakati wa maandamano ya Gen Z na Azimio. Kwa sasa hatuelewi kinachoendelea,” akasema Bw Osotsi.
Seneta huyo wa Vihiga alisema chama hicho hasa kimeshughulishwa na serikali kuendelea kuvunja haki, akirejelea tukio la juzi ambalo lilihusisha wanafunzi wa Shule ya Wasichana wa Butere kule Nakuru.
“Hii ni kuadharau makubaliano tuliyoyaweka na ni suala ambalo tutakuwa tukishughulikia,” akasema Bw Osotsi.
Wiki jana, Raila alitoa wito kwa wanasiasa wa ODM wapunguze tofauti kati yao kuhusu utawala wa sasa na pia mkataba ambao walikuwa nao na UDA.