Habari za Kitaifa

Hali itaimarika 2024, viongozi waahidi raia sherehe za Mwaka Mpya zikifika kilele

January 1st, 2024 2 min read

Na WAANDISHI WETU

Wakenya na viongozi wao walikusanyika katika maeneo mbalimbali ya ibada na burudani kuukaribisha mwaka wa 2024 huku baadhi wakiwa na matarajio hali ya uchumi itaimarika na gharama ya maisha kupungua mwaka huu.

Gavana wa Kajiado Joseph Ole Lenku aliahidi kwamba serikali yake itatoa huduma bora 2024 huku akisema mwaka wa 2023 ulikuwa “mgumu”.

Katika ujumbe wake wa heri ya Mwaka Mpya, Bw Lenku alisema miradi ya maendeleo itazinduliwa na kuhakikisha kwamba wakazi wamepata huduma bora.

Alisema mwaka wa 2023 ulikuwa na changamoto tele haswa kiangazi cha kati ya 2000-2022 kilichosababisha mifugo kufariki.

“Mwaka wa 2023 ulikuwa mgumu kwa wakazi wa kaunti hii. 2024 utakuwa mwaka wa kutoa huduma kwa serikali yangu,”alisema Bw Lenku.

Viongozi wa Uasin Gishu wakiongozwa na Gavana Jonathan Bii, Seneta Jackson Mandago na mbunge wa Kesses Julius Rutto waliungana na waumini wa kanisa la AIC Fellowship katika mji wa Eldoret kukaribisha mwaka mpya.

Viongozi hao pia walilaumu upinzani kwa kutisha kuitisha maandamano wakisema utawala wa Kenya Kwanza unapaswa kupatiwa fursa la kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Inasikitisha sana kwamba baadhi ya viongozi wanafikiria kuwaongoza watu kuandamana sasa wakati uchumi wetu unaimarika polepole, mwaka huu wa 2024 tunapaswa kukataa maandamano,” alisema Gavana Bii.

Viongozi hao walitoa wito kwa upinzani kufikiria kutumia njia mbadala kukosoa serikali.

“Hakuna uchumi tofauti kwa wale walio katika serikali na upinzani, tuna uchumi mmoja kama taifa la Kenya. Ni lazima sote tujitolee katika kuijenga nchi yetu. Nataka kumuomba rafiki yangu Raila Odinga kutojihusisha na shughuli zinazoturudisha nyuma,” akasema Seneta Mandago.

Katika Kaunti ya Turkana, Gavana Lomorukai na mwakilishi wa wanawake Cecilia Ngitit waliwaongoza wakazi kukaribisha Mwaka Mpya katika hoteli ya Stegra Hotel mjini Lodwar kwa maombi na matumaini ya maisha bora 2024.

Katika Kaunti ya Trans Nzoia, Wakenya wa matabaka mbali mbali walijazana katika maeneo ya ibada kukaribisha Mwaka Mpya huku wengine wakijumuika katika maeneo ya burudani.

Katika Kaunti ya Pokot Magharibi, Gavana Simon Kachapin aliahidi kuimarisha huduma kwa wakazi mwaka wa 2024.

Na huko Kilifi, Gavana Gideon Mung’aro aliandaa hafla katika mji wa Malindi kuukaribisha Mwaka Mpya katika ufuo wa Buntwani.

Miongoni mwa wasanii waliotumbuiza huko ni Susumila, Dragon Boys, Babu Vengi, Young Voice, Skill T miongoni mwa wengine.

Hafla hiyo iliisha kwa fataki za kukaribisha mwaka zilizopigwa pindi tu ilipogonga saa sita usiku.

Kwenye Bustani ya Mama Ngina Water Front jijini Mombasa, Gavana Abdulswamamd Nassir aliandaa sherehe iliyowaruhusu kila mkazi kuhudhuria, fataki zote zilipigwa kukaribisha mwaka wakazi wakizistaajabia kwa imani ya kuwa mwaka utakuwa bora zaidi.

Ripoti Za Stanly Kimuge, Alex Kalama, Stanley Ngotho, Oscar Kakai, Evans Jaola na Jurgen Nambeka