HabariHabari za Kaunti

Hofu wasichana wadogo wakikumbatia ukahaba Lamu

Na KALUME KAZUNGU August 11th, 2024 2 min read

SHIRIKA la Wanawake la Lamu Women Alliance (LAWA) limefokea baadhi ya mabinti ambao wameanza kuingilia ‘kazi’ ya ukahaba kisiwani Lamu kwa kile wanachodai kuwa ni hali ngumu ya maisha.

Afisa Mtendaji wa LAWA, Bi Raya Famau, alisema haipendezi kwa wanawake, hasa wale wa dini ya Kiislamu, kuingilia tabia hizo, hasa kwenye Mji wa Kale wa Lamu ambao unatambulika kuwa ngome kuu ya dini ya kiislamu.

Bi Famau alishikilia kuwa kuendeleza ukahaba ni sawa na kujishusha hadhi na hata kuharibu taswira nzuri ya kisiwa cha Lamu.

Badala yake, Bi Famau aliwasihi wanaobanwa na maisha kiasi cha kuingilia ukahaba wajitokeze hata kama ni kisiri kwa ofisi yake ili wajadiliane kuona ni jinsi gani watasaidiwa.

Afisa huyo kadhalika alisema ofisi yake iko tayari kukaribisha majadiliano na serikali ya kaunti na wadau mbalimbali kukabili mienendo hii.

Shirika hili liko mbioni kutambua na kutatua matatizo yanayowakumba wanawake yanayowalazimisha kuuza miili yao.

“Haileti picha nzuri kwa kisiwa cha Lamu kwamba ukahaba uendelezwe hata kama ni kwa kiwango kidogo namna gani. Cha msingi ni wahusika wawe wazi, wajitokeze tusemezane kabla ya kuwasaidia kuepuka kuuza miili yao na hata kujishusha hadhi. Hakuna lisilowezekana kama nia ipo,” akasema Bi Famau.

Kauli ya Bi Famau inajiri wakati ambapo wazee na viongozi wa dini ya Kiislamu kisiwani Lamu tayari wamejitokeza kulaani vikali biashara ya ukahaba kuingizwa eneo hilo.

Mwenyekiti wa Baraza Kuu la Waislamu Nchini (SUPKEM) tawi la Lamu, Bw Mohamed Abdulkadir alisema haya yanajiri sababu ya mwingiliano wa kijamii.

SUPKEM inasema jamii mbalimbali ambazo zimeingia eneo hilo miaka ya hivi karibuni zimeleta tabia geni kisiwani pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii.

Ikumbukwe kuwa mji wa kale wa Lamu ni kitovu cha Waswahili wa Jamii ya Wabajuni ambao dini yao huwa ni Uislamu.

“Hizi tabia hazijakuwepo miaka ya nyuma. Tabia hizi za kuoza zinachangiwa na mitandao ya kijamii kama vile TikTok, Instagram, Twitter (X), Facebook na mingineyo. Utapata wasichana wakijianika nusu-uchi mitandaoni na hata kushiriki ukahaba usiku ambalo ni suala la kuvunja moyo. Twalaani vitendo hivyo,” akasema Bw Abdulkadir.