Habari

JAMVI: Dai litamjenga au litambomoa?

June 30th, 2019 3 min read

Na BENSON MATHEKA

MADAI ya Naibu Rais William Ruto kwamba baadhi ya mawaziri na makatibu wa wizara kutoka Mlima Kenya walikutana kupanga njama za kumuua, yanaweza kuwa pigo kwake kisiasa ikibainika sio ya kweli na kumjenga pakubwa ikigunduliwa ni kweli, wadadisi wanasema.

Kufikia sasa, Dkt Ruto hajaandikisha taarifa kuhusu madai hayo na wapelelezi wanasema itakuwa vigumu kwao kuanza uchunguzi bila taarifa yake.

Kulingana na waziri wa viwanda, Bw Peter Munya, Dkt Ruto alieleza wapelelezi kwamba mawaziri wanne kutoka Mlima Kenya wamekuwa wakikutana katika hoteli ya La Mada kwenye barabara ya Thika, kupanga njama ya kumuua.

Bw Munya aliyeandamana na wenzake Sicily Kariuki na Joe Mucheru alisema kwamba mikutano yao katika hoteli hiyo ilihudhuriwa na zaidi ya watu 40 na ilikuwa ya kujadili miradi ya maendeleo katika eneo lao na sio kupanga njama ya mauaji.

Siku moja baada ya mawaziri hao kufika katika makao makuu ya upelelezi na kukataa kuandikisha taarifa kwa sababu Dkt Ruto hakuwa ameandikisha yake kama mlalamishi, Katibu wa Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho aliandikisha taarifa akitaka Naibu Rais achunguzwe.

Baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuwa Dkt Kibicho alilalamika kuwa Dkt Ruto na washirika wake wa kisiasa wamekuwa wakimnyanyasa akitekeleza majukumu yake.

Wadadisi wanasema iwapo barua iliyodaiwa kuandikwa na mmoja wa mawaziri kufichua njama za kutaka kumuua Dkt Ruto itabainika kuwa feki, madai hayo yatakuwa pigo kwa naibu rais.

“Itachukuliwa kuwa alikuwa na nia mbaya dhidi ya mawaziri hao na maafisa wa serikali kwa jumula na itakuwa pigo kwake kisiasa hasa kwa sababu alikuwa amepenya eneo la Mlima Kenya na kupata umaarufu mkubwa kwa kuzindua miradi ya maendeleo na kuchanga pesa,” alisema mwanasiasa mmoja wa chama cha Jubilee ambaye aliomba tusitaje jina lake kwa sababu za kibinafsi.

Idara ya upelelezi wa Jinai imewaalika wapelelezi kutoka Amerika, maarufu kama FBI kuchunguza barua iliyosambazwa mitandaoni na ambayo wachunguzi wa humu nchini wanashuku kuwa ni feki.

Wadadisi wanasema kwa kuwaalika FBI, Mkurugenzi wa Upelelezi wa jinai nchini George Kinoti anataka kuondoa lawama zozote kutoka upande wa Dkt Ruto ambaye amekuwa akilaumu idara yake kwa kutumiwa kutimiza malengo ya kisiasa.

Kulingana na mwanasiasa huyo, iwapo itabainika madai hayo si ya kweli, itachukuliwa kuwa Dkt Ruto anawachukia mawaziri na maafisa wa serikali kutoka Mlima Kenya ambao Rais Kenyatta anawaamini.

“Ikigunduliwa kuwa madai hayo ni feki, wapigakura wa eneo la Mlima Kenya ambao wamekuwa wakimkumbatia Dkt Ruto watakosa imani naye. Aidha, uhusiano wake na Rais Kenyatta unaweza kuathirika zaidi ikizingatiwa kwamba mawaziri na maafisa waliotajwa wanatoka ngome yake ya kisiasa,” aeleza mchanganuzi wa kisiasa, Peter Wanyama.

Mdadisi huyo anasema kwamba Dkt Ruto analenga kura za eneo la Mlima Kenya kuweza kufanikisha azma yake ya kuwa rais 2022 na matokeo ya uchunguzi yanaweza kumpiga jeki au kumpiga kumbo kisiasa.

“Ikibainika madai hayo ni ya kweli, Dkt Ruto atapata ujasiri wa kupenya maeneo mengine kisiasa lakini kwa kila hali yataathiri uhusiano wake na Mlima Kenya,” asema Bw Wanyama.

Kuna hisia kwamba kwa kulaumu mawaziri na makatibu kutoka Mlima Kenya, Dkt Ruto alikuwa akimlenga Rais Kenyatta ambaye anawaamini sana na ambaye, kulingana na Bw Munya, aliwaagiza wawe wakikutana na viongozi wa eneo hilo kupokea malalamishi kuhusu maendeleo na kutafuta jinsi ya kuyashughulikia.

Ruto huenda akabadilisha mwelekeo

Mwandani mmoja wa Dkt Ruto ambaye aliomba tusitaje jina lake anasema madai hayo yanaweza kumfanya Naibu Rais kubadilisha mwelekeo wake kisiasa kama hatua moja ya kujijenga kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022.

“Anajua amewekewa na anaendelea kuwekewa vikwazo na lazima atafute njia za kuviruka. Anajua kwamba ni mlima kupata kura za eneo la Mlima Kenya na hivyo sharti mtu ajipange,” aeleza.

Sio siri kwamba Dkt Ruto amefaulu kujenga umaarufu wake eneo la Mlima Kenya kupitia miradi ya maendeleo na kujishindia wabunge kadhaa vijana walio na ushawishi wanaomuunga mkono.

Inasemekana kuwa wanamikakati wa Dkt Ruto wamefaulu kuteka baadhi ya viongozi na wapigakura kutoka Mlima Kenya kupitia propaganda mashinani kwamba eneo lao limetengwa kimaendeleo.

Hii ilizindua wandani wa Rais Kenyatta ambao walianza kuweka mikakati ya kufanikisha miradi ya maendeleo eneo hilo bila kumhusisha Dkt Ruto.

“Kwa kufanya hivi, walilenga kuzima kwa kiasi kikubwa ziara za Dkt Ruto kuzindua miradi ya maendeleo eneo hilo ambayo alitumia kujijenga kisiasa,” aeleza Victor Kamau, mdadisi wa siasa.

Anasema ikiwa maelezo ya Bw Munya kwamba mikutano yao ilikuwa na ‘baraka’ za Rais Kenyatta ni ya kweli na ikibainika barua inayochunguzwa ni feki, Dkt Ruto atakuwa amejikwaa kisiasa eneo la Mlima Kenya.

“Wapinzani wake wa kisiasa watakuwa na sababu ya kumponda kwa kutoa madai ya uongo. Cheche za siasa zitatanda ikidaiwa kwamba anachukua watu kutoka eneo fulani,” asema Bw Kamau.

Wadadisi wanasema japo usalama wake umeimarishwa, haitakuwa rahisi kwa Dkt Ruto kuzuru maeneo tofauti ikiwa madai hayo ni ya kweli.

“Naona anaweza kupunguza ziara zake hasa katika maeneo ambayo anahisi usalama wake utakuwa hatarini,” anasema Bw Wanyama.