Habari za Kaunti

Joho aonya kampuni za uchimbaji madini zinazokiuka sheria

Na LUCY MKANYIKA  August 17th, 2024 2 min read

WAZIRI wa Madini Hassan Joho ametoa onyo kwa wachimbaji madini wanaokosa kutimiza majukumu yao ya maendeleo ya jamii kulingana na sheria ya uchimbaji madini. 

Akiongea katika eneo la Kishushe, Kaunti ndogo ya Wundanyi, Kaunti ya Taita Taveta, Bw Joho alisema kuwa wawekezaji kutofuata sheria kumenyima serikali na jamii manufaa yanayotokana na sekta hiyo.

Alisema kuwa sekta ya madini ina nafasi ya kuchangia katika Pato la Taifa (GDP), lakini baadhi ya wawekezaji wamekuwa wakishindwa kuzingatia sheria kwa kulipa ada zinazohitajika hivyo kuinyima serikali kodi.

“Serikali haitawavumilia wawekezaji wa aina hiyo. Wawekezaji wanaofanya kazi bila kutimiza sheria inayotakiwa kama vile kufanya maendeleo kwa jamii, kiboko chao ki motoni,” alisema.

Waziri huyo vile vile aliwaonya maafisa wa idara ya Madini na kuwaagiza wahakikishe kuwa wachimbaji wakubwa na wachimbaji wadogo wanapewa usaidizi unaohitajika kufanya kazi yao ili iwe na faida.

Alisema kuwa wachimbaji wadogo pia wana haki ya kusikizwa jinsi wale wakubwa wanavyopewa kipaumbele.

“Nataka nitoe onyo kwamba hii ni mara ya mwisho kwa watu wawili kuwekwa kwenye eneo moja la uchimbaji, pia sitaki kusikia mchimbaji ameanza kazi bila kupata ruhusa kutoka kwa jamii au wamiliki wa ardhi,” alisema.

Aidha, alisema wizara yake itatunga sheria itakayowalazimu wawekezaji kulipa kwanza ushuru unaohitajika kabla ya kuuza madini yao ili kuepusha serikali kukosa mapato.

Waziri Joho alikuwa akiongea wakati wa mkutano wake rasmi wa kwanza tangu aingie ofisini, ambapo alitembelea eneo la Kishushe ili kutatua mzozo unaoendelea kati ya jamii hiyo na kampuni ya Samruddha Resources Kenya Limited.

Kampuni hiyo, inayochimba madini ya chuma katika ranchi ya Kishushe, imekuwa ikizozana na jamii na wenye ranchi kwa kushindwa kulipa deni la Sh30 milioni lililokuwa likikusudiwa kwa miradi ya jamii katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita.

Waziri Joho aliwasilisha hundi ya mwisho ya Sh10 milioni iliyokusudiwa kutimiza sehemu ya majukumu yake ya kijamii (CSR) baada ya mwekezaji kulipa deni hilo wiki jana.

Fedha hizo zilikabidhiwa kamati ya jamii hiyo, ambayo inatazamiwa kufanya vikao vya umma ili kuwapa fursa wakaazi kupendekeza miradi yao.

Waziri Joho aliihimiza kamati hiyo kutumia fedha hizo kwa uadilifu, akitaka kuwepo kwa uwazi na uwajibikaji.

Hivi majuzi, kampuni ya Samruddha ilitangaza kuwa itarejea kazini baada ya takriban miaka minne baada ya kufungwa kwa mgodi huo.

Katibu Mkuu wa Madini Bw Elijah Mwangi alisema kamati nyingine itaundwa na kutangazwa kwenye gazeti rasmi la serikali.

Vilevile, alisema kuwa serikali itahakikisha kuwa wenyeji wananufaika kwa madini yanayopatikana katika eneo hilo.

Mbunge wa Wundanyi Bw Danson Mwashako pia alitoa wito wa kusuluhisha masuala ya usimamizi katika ranchi hiyo, ambapo mirengo miwili inadai uongozi ili kuhakikisha kuwa shughuli za uchimbaji madini zinanufaisha jamii za eneo hilo katika Kaunti ya Taita Taveta.

“Wananchi wa eneo hili wamekuwa wakiteseka ilhali wana rasilimali nyingi, watu wengine wana nia ya kuwafanya maskini licha ya kuwa na rasilimali nyingi,” alisema.

Kwa upande wake, Naibu Gavana Christine Kilalo amewataka wananchi kukumbatia wawekezaji ili wanufaike na rasilimali zao.

“Hatutaki kuwa na rasilimali ambazo hazitunufaishi. Wawekezaji wamekuwa wakisafirisha madini yetu nje ya nchi lakini hatujaona manufaa yake,” alisema.