Habari za Kitaifa

Kahawa: Mageuzi yanalenga ubora licha ya changamoto za uzalishaji   

June 11th, 2024 2 min read

NA SAMMY WAWERU

MAGEUZI yanayoendelea katika sekta ya kahawa yanalenga kuleta ubora na mapato kwa wakulima, licha ya takwimu kuonyesha kiwango cha uzalishaji kimeshuka, serikali imesisitiza.

Data za Mamlaka ya Kahawa nchini zinaonyesha kiwango cha mazao ya kahawa kimeshuka hadi Tani Metri (MT) 48, 649 mwaka 2022/2023, kutoka 51, 853 (2021/2022).

Kwenye ripoti kuainisha hatua zilizopigwa kupitia mageuzi katika sekta ya zao hilo linalotajwa kuwa ‘dhahabu nyeusi’ yanayoongozwa na Naibu wa Rais Rigathi Gachagua, kabla na baada, takwimu za mamlaka hiyo ya kiserikali hata hivyo zinaonyesha kiwango che eneo linalolimwa kimeongezeka kutoka 109, 385Hekta hadi 111, 902.

Mwaka mmoja tangu Bw Gachagua atwikwe jukumu kuongoza kuleta mabadiliko katika sekya ya kahawa, majanichai na ile ya maziwa, serikali inasisitiza kuwa ni mapema kupima utendakazi wa mageuzi yanayotekelezwa.

Akizungumza jana kwenye kikao na wanahabari jijini Nairobi, Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogondogo na za Kadri (MSME), Simon Chelugui alisema licha ya kupungua kwa kiwango cha uzalishaji wa kahawa nchini, mageuzi yanayoendelea yanapania kuleta ubora katika sekta.

“Wakulima wanakandamizwa sana katika soko la kahawa, na hatutalegeza kamba mageuzi tuliyoanzisha,” Bw Chelugui akasema.

Alisema mikakati ya serikali inalenga kuleta tabasamu katika sekta ambayo awali ilikuwa fahari ya Kenya ulimwenguni.

Mwaka uliopita, 2023, kongamano la kwanza lilifanyika katika Kaunti ya Meru ambapo wadauhusika katika sekta walitoa mseto wa mapendekezo, yanayoshirikisha kubuniwa kwa Mswada wa Kahawa 2023, wa Vyama vya Ushirika 2o23 na Sheria za Biashara 2023 katika Soko la Ubadilishanaji Hisa za Kahawa Nairobi (NCE), kati ya mengine.

Miswada mingine serikali inapania kutilia mkazo ni Crops (Coffee) General Regulation 2019 na Capital Markets (Coffee) Exchange 2020.

Waziri aliambia wanahabari kuwa mageuzi yanayoendelea yameashiria kuleta afueni katika kutunza mkulima wa kahawa, akitaja kutathmini leseni za wanaosaga mazao, mawakala na maajenti, wauzaji na mabohari, kuongezeka kwa kiwango cha mauzo NCE, kupanda kwa kiwango cha usambazaji wa fedha kuboresha ukuzaji wa kahawa (Coffee Cherry Advance Revolving Fund – CCARF), kuimarika kwa mifumo ya malipo na kupanuka kwa masoko ya kitaifa, kama hatua murwa za maendeleo zinazotokana na hatua ya serikali.

Kahawa ya Kenya inanadiwa kupitia NCE na Mfumo wa Moja kwa Moja kwa wanunuzi ng’ambo.

Mpango wa fedha kuboresha kilimo cha kahawa ulizinduliwa Februari 2020, na kufikia sasa mgao wake umefikia kima cha Sh6.7 bilioni.

Fedha hizo zinazambazwa kwa wakulima kupitia Shirika la New KPCU.

“Safari kuboresha sekta ya kahawa inalenga kuinua maisha ya wakulima, na ni mojawapo ya nguzo kuu katika Mpango wa Kuinua Uchumi kutoka Chini kuelekea Juu (BETA),” Bw Chelugui alifafanua.

Data za Mamlaka ya Kahawa nchini zinaonyesha mapato ya wakuzaji yaliongezeka kwa asilimia 12 chini ya mageuzi yanayoendelea, kiwango cha mauzo 2021/2022 kikipanda kutoka 42, 858MT hadi 47, 957 katika mauzo ya 2022/2023.

Ripoti ya sasa, 2023/2024, kufikia Mei 2024 jumla ya magunia 496, 505 yameuzwa kupitia soko la kunadi, idadi hiyo ikiwakilisha 30, 477MT.

Idadi jumla ya mauzo ng’ambo, nayo inasimamia 21, 978.19MT, huku mauzo ya moja kwa moja yakiwa 822.16MT.

Kwenye kikao na wanahabari jana, Bi Wanjiku Wakogi, Mkuu wa Utumishi wa Umma katika Afisi ya Naibu Rais, alihimiza wadauhusika kushirikiana ili kufanikisha ajenda ya mageuzi.

“Tukishirikiana tutafanikiwa, na la mno tuzamie uongezaji kahawa thamani kusaka masoko yenye ushindani mkuu,” alihimiza.

Amerika, Ubelgiji na Ujerumani, ndio wanunuzi wakuu wa kahawa ya Kenya.

Zaidi ya familia 800, 000 zinategemea kilimo cha kahawa, zao hilo likikuzwa katika kaunti 32.

[email protected]