• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Kamanda Francis Kooli: Afisa tajiri wa utu na moyo kuhudumia jamii

Kamanda Francis Kooli: Afisa tajiri wa utu na moyo kuhudumia jamii

NA JESSE CHENGE

MJI wa Bungoma, ulioko eneobunge la Kanduyi ni wenye shughuli tele na ni katika eneo hilo tunakutana na afisa wa polisi mwenye huduma za kipekee.

Kando na jukumu alilotwikwa na mwajiri wake (NPS) kulinda wananchi, wenyeji wa anakohudumu wana kila sababu ya kutabasamu kufuatia upekee wake kiutendakazi na maafisa anaosimamia.

Si mwingine ila ni Francis Kooli, Kamanda wa Polisi Kaunti ya Bungoma.

Anaamini kuwa kutumikia jamii sio tu kukamata watu na kuwasukuma gerezani.

Kinachoridhisha zaidi kuhusu afisa huyu, ni moyo wake wenye ukwasi wa ukarimu ambapo husikiliza upande wa wanaojipata kuandamwa na sheria, kutoa msaada, ushauri na mawaidha kukwepa kukwaruzana na sheria.

Akiwa na ufasaha kuporomosha lugha ya Kiswahili na Kiingereza, Bw Kooli anaamini sana kuwa kutumikia jamii sio tu kukamata watu na kuwasukuma gerezani.

“Wakala wa kisasa wa polisi hutendea kila mtu kwa utu na heshima, wakitumia ujuzi wa kibinadamu na huruma. Ni rahisi kupata maneno sahihi kwa mwathiriwa wa uhalifu, lakini hakuna sababu ya kutomtendea kila mtu kwa neema, hata kama nguvu ya kimwili inahitajika,” anasema.

Kwake, polisi ni umma na umma ni polisi.

Lakini, kinachomtofautisha Bw Kooli na wengine ni shauku ya kuwasaidia wengine katika jamii.

Francis Kooli, Kamanda wa Polisi Bungoma akisaidia mkazi mwenye hitaji la kimsingi. Picha|JESSE CHENGE

Anaamini kwamba polisi hawana lengo la kuwakamata wahalifu tu, bali pia kusikiliza na kusaidia jamii.

Afisa huyu ni mzaliwa wa Kaunti ya Turkana ambako pia amekulia.

Amehudumu katika Idara ya Polisi kwa muda mrefu, na amepanda ngazi hadi kuwa Kamanda wa Polisi Kaunti.

Kutembea mamia ya kilomita kuhamasisha uchangiaji damu

Mwamka 2011, Kooli alisafiri zaidi ya kilomita 250 kuhamasisha Wakenya kuchanga damu, hatua iliyosaidia ukusanyaji wa painti 2, 683.

“Tulitembea kutoka Kakamega hadi Nakuru tukihamasisha Wakenya kutoa damu ili kusaidia wagonjwa wenye upungufu,” Kooli asema.

Alijiunga na Idara ya Polisi 1993, na amehudumu katika Kaunti za Isiolo, Nakuru, Kakamega, Laikipia, Bomet, Migori, Kisii na Bungoma.

Mojawapo ya miradi miradi anayotarajiwa kuzindua Bungoma Agosti 2023, ni mpango kuunda ukuta katika msitu wa Mlima Elgon, moja ya minara kuu ya maji eneo hilo.

Kamanda wa Polisi Bungoma, Bw Francis Kooli akiwapa mawaidha na ushauri wanafunzi. Picha|JESSE CHENGE

Msitu huo ni makazi ya wanyamapori na mimea asilia, ambayo ni muhimu kwa uhifadhi wa bayoanuwai.

Kwa kutumia mfumo wa jua, Kooli anatumai kulinda mnara wa maji na msitu dhidi ya uvamizi wa binadamu na uharibifu wa makazi.

Mpango wa Kooli ni ushahidi wa kujitolea kwake kutumikia jamii na kuleta matokeo chanya kwa mazingira.

Afisa huyu anaamini kwamba sote tuna wajibu wa kurudisha na kuifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi, tendo moja dogo la fadhili kwa wakati mmoja.

Bw Kooli ataendelea kuhimiza askari na mashirika ya kuhifadhi mazingira katika Kaunti ya Bungoma kupanda miti Mlima Elgon kwa lengo la kuongeza misitu.

Kibarua kingine kinachomsubiri ni kuimarisha usalama eneo la Chepkitale, Mlima Elgon ambapo ameratibiwa kuanzisha kituo cha polisi.

  • Tags

You can share this post!

Makahaba Tana River watangaza nyongeza ya bei ya huduma za...

Raila Odinga alivyoingia jijini Nairobi kwa staili na kuapa...

T L