Habari za Kaunti

Kaunti yakasirishwa na tabia za shule kutoza wazazi ada haramu wanafunzi wa chekechea wakifuzu

Na SHABAN MAKOKHA September 22nd, 2024 1 min read

KAUNTI ya Kakamega imepiga marufuku sherehe za kufuzu kwa wanafunzi wa chekechea katika shule zote za umma ikidai zinatumika kukama wazazi hela zao.

Walimu 1,631 ambao wanafundisha katika shule hizo za chekechekea wametakiwa wasikusanye pesa kutoka kwa wazazi kuandaa sherehe hizo.

Kwenye memo iliyotumwa  na Afisa Mkuu wa Elimu wa Kakamega Viviane Ayuma, sherehe hizo sasa ni haramu katika gatuzi hilo.

“Tumegundua kuwa shule zinapanga kuandaa sherehe hizo na sasa tumezipiga marufuku,” akasema Bi Ayuma huku akiamrisha maafisa wa elimu nyanjani wahakikishe kuwa uamuzi huo unatekelezwa.

Haya yanajiri wakati ambapo wazazi wamelalamika kuwa wasimamizi wa shule za chekechea wanashirikiana na walimu wakuu kuwapunja hela kupitia sherehe hizo.

Wazazi walisema kuwa sasa wanatozwa kati ya Sh1, 500 hadi Sh2, 000 kama ada kwa wanafunzi wa madarasa ya chekechea wanaotarajiwa kufuzu.

Huku akisema sherehe hizo hazitaandaliwa shule zikifungwa, Bi Ayuma alisema zinaenda kinyume na msimamo wa kaunti ambayo inafadhili elimu hiyo.

“Kaunti imekuwa ikitoa elimu ya bure katika shule za chekechea na si vyema iwapo wazazi bado watakuwa wakitakiwa walipe pesa za watoto kwenye shule za chekechea kufuzu,” akaongeza Bi Ayuma.

Kaunti imekuwa ikilipa Sh1, 000 kwa kila mwanafunzi katika shule ya chekechea.

Pia imekuwa ikinunua ardhi ambapo shule hizo huanzishwa na kununua samani na vifaa vingine vya masomo.

Kaunti pia imekuwa ikishirikiana na mashirika kama USAID, World Vision, UNICEF na Shirika la Walemavu la Chesire kutoa mafunzo ya malezi kwa walimu.

Pia kupitia ushirikiano huo, madarasa yamekuwa yakijengwa na wanafunzi kupewa vifaa vya masomo.