Makala

Kazi ya kuwasilisha chupa moja ya pombe kwa mteja yaishia mauti

May 26th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Aprili 23, 2024, James Muturi Gathaiya akiwa yatima wa umri wa miaka 38 alipata kazi ya kuwasilisha chupa moja ya pombe katika boma moja lililoko katika mtaa wa Thika Greens, Kaunti ya Murang’a.

Chupa hiyo ikiwa ya pombe aina ya Chrome ya kipimo cha 250 milimita ilikuwa imegharimu Sh350 na ikawa ndio kiini cha Muturi kufikwa na mauti.

Aliangamia kikatili lakini sasa inadaiwa maafisa wanaofaa kuisadia familia yake, wanafunika haki.

Muturi alikuwa ameenda kupumzika katika duka moja la kuuza pombe na mvinyo lililo karibu na nyumba ya aliyeagiza chupa hiyo moja.

Kwa kuwa aliyekuwa ameagiza alikuwa jirani yake, mhudunu wa duka alimpa Muturi nafasi hiyo ya kuwasilisha ili alipwe Sh50.

Kile Muturi hakujua ni kwamba, aliyekuwa ameagiza pombe hiyo alikuwa ni kijana ambaye alikuwa ameachiliwa majuzi kutoka hospitali alikokuwa amelazwa akipambana na uraibu wa pombe na mihadarati.

Muturi aliingia katika boma hilo akiwa hana wasiwasi kwa kuwa katika nafsi yake, hakuwa na lolote la kumtia wasiwasi kwa kuwa alikuwa katika harakati tu za kawaida na kisha aende zake nyumbani akalale.

“Mimi nilikuwepo Muturi akipewa pombe hiyo kuipeleka hadi kwa boma lililoelezwa kuwa katika mtaa wa Nyumba ya Mzungu ulioko katika eneo III la mradi huo wa nyumba za Thika Greens,” asema Bw Frank Kiriinya.

Inadaiwa kwamba Muturi alifika katika boma hilo na yule mtu alikumbana naye nje ya nyumba ya alikokuwa ameagizwa kuwasilisha pombe, ni mamake mzazi kijana huyo.

Muturi akiwa hana habari, alimkabidhi mama huyo chupa hiyo ya pombe na ndipo ahera ya huku duniani ilimpasukia mbele yake kijana wa watu mwenye tu katumwa bila kuwa na habari ya mazingira halisi ndani ya boma hilo.

“Kufungua na kuona ilikuwa ni pombe, mama huyo alipiga nduru na akawaita walinzi ambao walikuwa katika lango kuu la kuingia katika mtaa huo. Alipiga nduru akisema kwamba alikuwa amempata mlanguzi wa mihadarati ambaye alikuwa kiini cha uraibu wa kijana wake,” asema mlinzi mmoja ambaye hakutaka kutanjwa.

Mlinzi huyo akihojiwa na Taifa Jumapili alidai kwamba mama huyo hata alitoa Sh5,000 kama mshahara kwa walinzi hao ili ‘wampe funzo’ Muturi.

“Ni baada ya kuona kwamba Muturi alikuwa katika hatari ya kuuawa ambapo nilipiga simu kwa mama ambaye alikuwa amemwajiri kazi. Ilikuwa dhahiri kwamba walinzi hao walikuwa wameamua kumuua mwanamume huyo na ndipo nikaona tu nijaribu kumnusuru,” asema mlinzi huyo.

Bi Joyce Ndirangu ambaye alimchukua Muturi kama mfanyakazi wake mwaka wa 2018 alisema kwamba alipokea simu hiyo mwendo wa saa moja na ndipo akamtuma kijana wake aende akajue hali ilikuwa aje.

Anasema kwamba kijana huyo alifika eneo hilo na akapiga simu akimmfahamisha kwamba “Muturi alikuwa akipigwa kama nyoka na alikuwa akihitaji uokozi wa dharura”.

Kwa kuwa ilikuwa vigumu kuingia katika boma hilo ambalo Muturi alikuwa akipigiwa, kijana huyo alisubiri hadi walinzi hao walipopewa amri ya kutamatisha kipigo hicho cha adhabu.

“Walinzi walisema hakuna vile wangemtoa Muturi wakimbeba hadi kwa lango kuu kwa kuwa kuna kamera za siri. Ndipo uamuzi uliafikiwa wa kumweka ndani ya gari na kisha kumtoa nje na ambapo walimweka katika matuta ya barabara akiwa hoi,” asema mlinzi mdokezi wa kisa hicho.

Mama huyo mwenye kufadhili kipigo hicho anasemwa kwamba alipiga simu nyingine na muda baadaye kukatokea gari ambalo lilimkanyaga Gathaiya kwa mbavu na miguu, likarudi nyuma tena likimponda na kisha likampitia juu kwa mara ya tatu.

Baada ya dakika nyingine kadha, kulitokea gari la polisi ambalo lilibeba mwili wa Muturi na kuupeleka katika mochari ya General Kago.

Bw Kennedy Kimathi ambaye alijitambulisha kama rafiki wa muda mrefu wa Muturi kutoka utotoni wao katika kijiji cha Kaunti ya Nakuru, alisema kwamba alifika katika mochari hiyo kuutambua mwili lakini akapata kwamba mwili huo ulikuwa ukilindwa na polisi na ambao walikuwa na amri kwamba kusikubaliwe yeyote bila idhini ya wakubwa wa polisi kuuona.

Bw Kimathi anasema kwamba kulikuwa na afisa mmoja wa kitengo cha polisi wa trafiki ambaye alikuwa akitoa onyo mara kwa mara kwamba ni lazima mwili huo wa Muturi ungezikwa haraka iwezekanavyo.

Bw Kimathi anaongeza kwamba maafisa hao walikuwa wakikiri hadharani kwamba “wale waliohusika katika mauti ya Muturi walikuwa wakubwa na hakuna mahali ambapo wangepelekwa na yeyote”.

Maafisa hao hata walijitolea kutoa pesa za kugharimia mazishi ya Muturi baada ya kuambiwa kwamba alikuwa yatima na bila watu walio na uwezo wa kumudu gharama.

Waombolezaji siku ya mazishi ya James Muturi Gathaiya. PICHA | MWANGI MUIRURI

Daktari wa upasuaji miili, John Mathaiya ambaye alitekeleza jukumu hilo mnamo Mei 2, 2024, katika mochari ya General Kago aliambia Taifa Jumapili kwamba “niliyonakili kama matokeo ya upasuaji huo yaliorodheshwa na maafisa wa polisi kama siri ya kiusalama na ninaweza tu nikaongea kuyahusu kupitia wito wa mahakama au wa ilani yake”.

Kwa mujibu wa ripoti ya uchunguzi ambayo Taifa Jumapili iliona katika kamati ya kiusalama ya Kaunti ndogo ya Gatanga, “marehemu Muturi aliaga dunia kupitia ajali mbaya ya barabarani na ambapo gari lililomuua linasakwa”.

Ripoti hiyo haitaji lolote kuhusu ununuzi wa pombe, uwasilishaji wayo katika boma hilo, shambulio dhidi ya Gathaiya na kisha kutupwa hadi kubebwa kwa gari hadi kwa barabara.

Hii ni licha ya Bw Kiriinya na Bw Kimathi pamoja na mashahidi wengine kujitolea kuandikisha taarifa za kulalamikia mauaji ya Muturi.

Kamishna wa Kaunti ya Murang’a Bw Joshua Nkanatha alisema kwamba alipata habari kuhusu utata unaozingira kifo cha Muturi.

Kamishna wa Murang’a Joshua Nkanatha. PICHA | MAKTABA

“Nimetoa mwelekeo kwamba kuandaliwe ripoti rasmi katika kikao cha Kamati ya Usalama ya Kaunti. Tayari kuna maafisa ambao wanashughulikia suala hilo na natoa hakikisho kwamba hali halisi ya kisa hicho itajitoa na kisha mkondo wa haki ujidhihirishe,” akasema Bw Nkanatha.

Alisema kwamba “sisi kama serikali hatuna haja yoyote ya kuficha ukweli kuhusu mauaji hayo na wote ambao watapatikana ni wenye lawama ya kuvunja sheria watawajibishwa vilivyo”.

[email protected]