Habari za Kitaifa

Kenya kurejelea kupeleka majanichai Tanzania baada ya vikwazo kuondolewa

February 15th, 2024 2 min read

NA BRIAN AMBANI

SERIKALI ya Tanzania imebatilisha uamuzi wa uagizaji wa majani chai kutoka nje, na kuwapa nafasi wafanyabiashara nchini kuanza tena kuuza bidhaa hiyo kwa nchi hiyo jirani.

Taarifa iliyotolewa Jumatano na Bodi ya majani Chai Tanzania, mdhibiti wa sekta ya chai nchini, ilisema itaanza tena kutoa vibali vya kuagiza bidhaa hiyo siku ya Jumatatu.

“Hii ni kukufahamisha kwamba utoaji wa vibali vya kuagiza bidhaa kutoka nje utaanza kutumika kuanzia Februari 19, 2024,” alisema mdhibiti katika taarifa iliyoelekezwa kwa wasindikaji wa chai na wafanyabiashara.

“Nyote mnakumbushwa kuzingatia kanuni na masharti yote kama yalivyoainishwa kwenye Sheria na Kanuni za Chai kabla na baada ya kuagiza bidhaa hiyo ili kuhakikisha kuwa mnafanya biashara ya haki na majani chai inawafikia watumiaji ukiwa na ubora unaokidhi viwango vya ndani na nje ya nchi,” ilisema.

Tanzania ilikuwa imesitisha utoaji wa vibali vipya vya kuagiza majani chai mapema mwezi huu kutokana na wasiwasi kuhusu masuala ya ubora.

Kenya imepongeza uamuzi wa Tanzania wa kurejelea utoaji wa vibali vya kuagiza bidhaa hiyo.

“Tunawashukuru kwa dhati wenzetu wa Tanzania kwa hatua hiyo muhimu,” alisema Katibu katika wizara ya Biashara Ombudo K’Ombudo kwenye mtandao wa X.

Kando na hayo, katibu huyo alisema kwamba nchi hizo mbili zitashirikiana ili kuendeleza biashara kati yao.

Hatua hiyo sasa itawawezesha wafanyabiashara wa majani chai nchini kusafirisha bidhaa yao Tanzania.

Hata hivyo, usafirishaji wa majani chai kutoka nchini hadi Tanzania bado ni mdogo lakini serikali ya Kenya imekuwa ikijitahidi kukuza mauzo yake nchini humo ili kuongeza mapato ya fedha za kigeni.

Kati ya maeneo 40 ya kuuza majani chai nchini mwaka 2022, Tanzania ilichukua kiasi kidogo zaidi cha shehena.

Mwaka 2022 kwa mfano, Kenya ilisafirisha kilo 1,200 tu za majani chai kwenda Tanzania, na kuifanya nchi hiyo kuwa ya mwisho kati ya nchi 40 ambazo Kenya ilisafirisha majani chai katika kipindi hicho.

Kwa sasa, Kenya inasafirisha bidhaa hiyo kwa nchi kama vile Pakistan, Misri, na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).