Makala

Kenya njia panda kuhusu mizozo na majirani wake

February 24th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

UBISHI mpya kati ya Kenya na Somalia kuhusu umiliki wa sehemu ya bahari iliyo na mafuta, umeibua maswali kuhusu hatua zinazopaswa kuchukuliwa na taifa hili kulinda mipaka yake, ikizingatiwa kuna mizozo ya mipaka kati ya Kenya na mataifa yote majirani.

Bali na mzozo wa Somalia ambao unashughulikiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), Kenya imekuwa ikizozania kisiwa cha Migingo kilicho katika mpaka wake na Uganda kwenye Ziwa Victoria, huku pia ikizozania eneo la Ilemi Triangle na Sudan Kusini.

Kwa upande mwingine, mizozo ya kimipaka imewahi kusababisha Tanzania kupiga mnada mifugo 1,325 wa raia wa Kenya na kwingineko Ethiopia, kumekuwa na matukio ya Wakenya kuvamiwa na raia wa Ethiopia mara kwa mara.

Viongozi na wataalamu wa masuala ya uhusiano wa kimataifa wanasema mizozo hii yote inastahili kutatuliwa haraka iwezekanavyo ili kuzuia uwezekano wa vita miaka ijayo.

Kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha Wakenya wanaoishi Ng’ambo, Dkt Shem Ochuodho, masuala haya yanahitaji kuchukuliwa kwa uzito.

Akitoa mfano wa Migingo, Dkt Ochuodho alieleza kuwa ni muhimu mambo kama haya yasuluhishwe wakati ambapo mataifa yangali yana amani na uhusiano bora, kwani itakuwa hatari zaidi kama kutaibuka tawala zinazopenda kutumia vita kutafuta suluhisho kuhusu mivutano na majirani.

“Inafaa mizozo hii ishughulikiwe kwani haitajitatua. Huenda kutakuja wakati ambapo tutapata serikali isiyoheshimu sheria na mambo yatakuwa mabaya zaidi,” akasema kwenye mahojiano jana.

Mzozo kati ya Kenya na Uganda kuhusu Kisiwa cha Migingo, kilicho na kiwango kikubwa cha samaki ulizidi wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Mwai Kibaki.

Ingawa mataifa hayo mawili yalitumia wataalamu kubainisha nchi inayomiliki kisiwa hicho, ripoti rasmi haijawahi kutolewa kwa umma na hadi leo raia wa Kenya wanaendelea kuhangaishwa na polisi wa Uganda licha ya kuwa kuna maafisa wa serikali ya Kenya katika kisiwa hicho. Hivi majuzi maafisa wa Uganda walishusha bendera ya Kenya kisiwani humo.

Mvutano kati ya Kenya na Somalia ulipelekea Wizara ya Mashauri ya Kigeni inayosimamiwa na Dkt Monica Juma, kutoa taarifa zenye ukali ikisisitiza kufanya kila iwezekanalo kulinda mipaka yake.

Hii ilishangaza wengi ambao wamezoea kuona taifa hili likitumia sera za kidiplomasia linaposhughulikia masuala mbalimbali ya kimataifa na inasubiriwa kuonekana hatua zitakazochukuliwa baadaye.

Mbunge wa Kandara, Bi Alice Wahome alisema Kenya imefahamika kihistoria kuwa taifa linalojali amani na majirani wake lakini majirani hawarudishi mkono kwa upole huo.

“Kuna wakati hata Wakenya hupigwa katika nchi jirani na inaonekana upole wetu unatumiwa vibaya,” akasema Bi Wahome alipohojiwa wiki iliyopita kwenye runinga ya NTV.

Kwa upande wake, Mbunge wa Kitutu Chache Kusini, Bw Richard Onyonka, ambaye amewahi kuwa Waziri Msaidizi wa Mashauri ya Kigeni, alitoa wito kwa Rais Uhuru Kenyatta aagize wizara hiyo ishirikiane na bunge la taifa kusuluhisha mizozo ya mipaka.

“Wizara inafaa kuwa na mikakati maalumu kutatua masuala tatanishi la mipaka. Sidhani kama ni vyema kuacha masuala haya bila kutatuliwa na kutumai suluhisho litajitokeza lenyewe,” akasema.