Habari za Kitaifa

Kenya yathibitisha kisa cha tano cha Mpox

Na CHARLES WASONGA September 6th, 2024 1 min read

WIZARA ya Afya imethibitisha kisa cha tano cha maambukizi ya Homa ya nyani (Mpox) nchini.

Mgonjwa huyo ni mwanamke mwenye umri wa miaka 29 anayeishi katika eneo la VOK, karibu na Tumaini Academy Mombasa.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari Ijumaa, Septemba 6, 2024, Waziri wa Afya Deborah Barasa alifichua kisa hicho kiligunduliwa Jumatano wiki hii na mgonjwa huyo yuko katika wadi maalum katika Hospitali ya Utange.

Dkt Barasa pia amefichua kuwa mgonjwa huyo ni mkewe mtu wa nne nchini kupatikana na virusi vya Mpox, ambaye amelazwa katika hospital moja mjini Nakuru anakopokea matibabu.

“Mgonjwa huyu wa tano hajawahi kuzuru nchini ambako kuna visa vingi vya Mpox, lakini mumewe juzi alisafiri hadi Rwanda na akarejea nchini Agosti 24, 2024. Uchunguzi unaendelea kubaini kuchipuka kwa visa vingine kwa lengo la kudhibiti msambao wa ugonjwa huu,” akaongeza Waziri Barasa.

Wakati huo huo, Waziri Barasa amesema kuwa kati ya sampuli 124 zilizopimwa kubaini ikiwa zina virusi vya Mpox, 110 hazikupatikana na virusi hivyo na sampuli tisa zingali zinachunguzwa.

Jumla ya wasafiri 687, 233 wamepimwa katika vituo 26 vya mpakani kama sehemu ya hatua za kudhibiti msambao wa Mpox.

Ugonjwa huo husambaa kupitia mtu kumgusa mwathiriwa, kutumia vifaa vyenye virusi vya Mpox na kugusa wanyama wanaoambukiza.

Ugonjwa huo pia unaweza kupitishwa kwa njia ya ngono.

Baadhi ya dalili zake ni, ongezeko la joto mwilini, kuumwa na misuli, kuumwa na mgongo na kutokwa na uvimbe sehemu kadhaa za mwili.